Vigogo kibao wanamtaka Nicolas
Muktasari:
- Taarifa zinaeleza Villa inapanga kumuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa England, Ollie Watkins, 30, mwisho wa msimu huu, hivyo inatafuta mbadala mapema.
ASTON Villa imejiunga rasmi kwenye mbio za kumsajili mshambuliaji wa Chelsea, Nicolas Jackson, 24, dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi.
Taarifa zinaeleza Villa inapanga kumuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa England, Ollie Watkins, 30, mwisho wa msimu huu, hivyo inatafuta mbadala mapema.
Jackson, ambaye hapati nafasi ya kudumu katika kikosi cha Bayern Munich ambako msimu huu anacheza kwa mkopo ameweka wazi hana mpango wa kurudi Chelsea baada ya mkataba wake na Bayern kumalizika hali iliyosababisha timu nyingi zianze kuulizia uwezekano wa kumsajili.
Mbali ya Villa, huduma ya Jackson pia inawindwa sana na AC Milan ambayo kwa sasa inatafuta washambuliaji inaoweza kuwasajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa ajili ya kuboresha safu yao ya ushambuliaji na miongoni mwa majina ambayo yapo katika orodha yao kwa sasa ni pamoja na Jackson, 24 na staa wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Guinea, Serhou Guirassy , 29.
Kwa sasa Jackson mwenyewe hajafanya uamuzi wowote juu ya wapi angependa kwenda kucheza ingawa inaaminika anaweza kutaka kubadilisha mazingira na kwenda Italia.
Marcus Rashford
MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Marcus Rashford amefikia makubaliano ya kusaini mkataba wa moja kwa moja wa miaka mitatu na Barcelona ambayo kwa sasa anaitumikia kwa mkopo wa msimu mmoja.
Barca inadaiwa kuwa tayari kulipa Pauni 26 milioni kuhakikisha inakamilisha uhamisho wa fundi huyu ambaye ameonyesha kiwango bora msimu huu. Awali dili hilo lilikuwa linaonekana kuwa na ugumu kukamilika kwa sababu Barca haikuwa tayari kutoa kiasi cha pesa kilichohitajika.
Rodri
MABINGWA wa kihistoria wa Ligi ya Ulaya, Real Madrid, bado ina mpango wa kumsajili kiungo wa Manchester City, Rodri mwenye umri wa miaka, 29, katika dirisha lijalo la usajili.
Inaripotiwa kuwa dili hilo linaweza kugharimu takribani Pauni 44 milioni, ingawa Manchester City hawako tayari kumuuza kirahisi mchezaji huyo muhimu.
Rodri ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2027, hivi karibuni amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.
Anthony Gordon
WINGA wa Newcastle United, Anthony Gordon, 25, ameendelea kuhusishwa na kujiunga na Arsenal, lakini taarifa mpya zinaeleza wazi Newcastle haina mpango wa kumuuza fundi huyu ambaye bado ana mkataba wa muda mrefu na timu hiyo.
Hata hivyo, uwezekano wa kuuzwa haujaondolewa moja kwa moja kwani taarifa kutoka Newcastle zimefichua timu hiyo inaweza kushawishika kumuuza ikiwa kuna ofa nono kuanzia Pauni 90 milioni.
Darwin Nunez
Atletico Madrid na Juventus zimeungana na Newcastle United kumwania mshambuliaji wa Liverpool, Darwin Nunez, 26. Nunez, ambaye kwa sasa anachezea Al-Hilal, ameripotiwa kuhitaji kurudi katika soka la kiushindani zaidi barani Ulaya hali inayochochea uwezekano wa kuondoka kwake. Hadi sasa hakuna timu iliyowasilisha ofa rasmi kwa ajili ya kumsajili lakini mazungumzo yanaendelea kufanywa baina ya wawakilishi wake na timu zinazomhitaji.
Randal Kolo Muani
MABOSI wa Juventus wameweka kipaumbele cha kumsajili mshambuliaji wa Paris Saint-Germain anayecheza kwa mkopo Tottenham Hotspurs, Mfaransa Randal Kolo Muani, 27, dirisha lijalo la usajili.
Kolo Muani kwa sasa yupo kwa mkopo Tottenham Hotspur akitokea Paris Saint-Germain na Juventus inaamini anaweza kuimarisha safu yao ya ushambuliaji msimu ujao. Juventus wanafuatilia kwa karibu maendeleo yake.
Marc Cucurella
ATLETICO Madrid bado inapambana kumsajili beki wa Chelsea, Marc Cucurella, 27, dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Cucurella, ambaye ana uwezo wa kucheza kama beki wa kushoto au winga anaweza akauzwa na Chelsea ambayo kwa sasa inapambana kuweka sawa hesabu zao ili kuepuka adhabu kutoka kwa mamlaka za soka England juu ya kukiuka kanunu za matumizi ya fedha.
Arne Engels
CELTIC ipo tayari kumuuza kiungo wao wa kimataifa wa Ubelgiji, Arne Engels dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambaye ilikataa kumwachia dirisha lililopita.
Inaelezwa Nottingham Forest iliwasilisha ofa ya Pauni 14 milioni ili kumsajili fundi huyo lakini ilikataliwa na Celtic iliyokuwa ikihitaji pesa nyingi zaidi, pia ilikuwa ngumu kumwachia Engels kwa sababu ingeharibu mipango ya timu kwa msimu huu.