Dusan Vlahovic aitamani FC Barcelona
Muktasari:
- Staa huyu amekuwa akiwindwa sana na Tottenham Hotspur and Chelsea zilizohitaji kumsajili tangu mwaka jana lakini ilishindikana.
MSHAMBULIAJI wa Juventus na timu ya taifa ya Serbia, Dusan Vlahovic anatamani zaidi kwenda Barcelona dirisha lijalo la majira ya kiangazi na mkataba wake utakuwa unamalizika.
Staa huyu amekuwa akiwindwa sana na Tottenham Hotspur and Chelsea zilizohitaji kumsajili tangu mwaka jana lakini ilishindikana.
Vlahovic mwenye umri wa miaka 26, haitaji kuendelea kubakia Juventus baada ya mkataba wake kumalizika na anahitaji changamoto mpya licha ya timu hiyo kumhitaji sana abaki.
Mkataba wa sasa wa Vlahovic unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 17 za michuano yote na kufunga mabao sita.
Ripoti zinaeleza Vlahovic yupo tayari hadi kupata mshahara pungufu ya ule ambao timu za England zimemwekea mezani ili tu kufanikisha dili la kwenda Barca kwa sababu ni miongoni mwa timu ambazo amekuwa akitamani kuzitumikia tangu akiwa mtoto mdogo.
Inaelezwa kwa sasa mazungumzo ya awali yanaendelea lakini hakuna mwafaka wowote uliofikiwa baina ya mabosi wa Barca na wawakilishi wa Vlahovic.
Murillo
LIVERPOOL bado inapambana kwa ajili ya kumsajili beki kisiki wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya Brazil, Murillo mwenye umri wa miaka 23, licha ya kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Chelsea ambayo pia inahitaji saini yake.
Murillo amekuwa akiwindwa na vigogo wa England tangu mwaka jana lakini mabosi wa Forest hawaonyeshi nia ya kumuuza ingawa raundi hii dili linaonekana kuwa na asilimia nyingi za kukamilika. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Honest Ahanor
ARSENAL na Manchester City zinadaiwa kuwa katika mpango wa kuwasilisha ofa kwenda Atalanta kwa ajili ya kumsajili beki wa kushoto wa timu hiyo, Honest Ahanor mwenye umri wa miaka 18.
Kwa mujibu wa ripoti Atalanta inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 30 milioni kwa ajili ya kumuuza Ahanour mwisho wa msimu. Mbali ya vigogo hao Chelsea pia ni miongoni mwa timu zinazohitaji huduma ya staa huyo wa kimataifa wa Nigeria.
Mateus Mane
LIVERPOOL na Manchester United zimekataa kulipa Pauni 50 milioni zilizohitajika na Wolves kama ada ya uhamisho ya kiungo wa klabu hiyo na timu ya taifa ya vijana ya England, Mateus Mane.
Ripoti timu hizo hazioni kama Mane ana thamani ya kiasi hicho cha pesa. Vigogo hawa walionyesha nia ya kumsajili staa huyu tangu Januari lakini Mane mwenyewe alikataa akiamini muda wake wa kuondoka bado haujafika na anahitaji kukua zaidi. Mkataba wa Mane unamalizika mwaka 2029.
Ivan Toney
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Brentford, Ivan Toney ana matumaini ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Saudi Arabia au kikombe akiwa na Al-Ahli lakini bado hajaondoa uwezekano wa kurejea katika Ligi Kuu England kwa msimu ujao.
Toney mwenye umri wa miaka 29, alidaiwa huenda angerejea England katika dirisha la usajili la Januari na yeye mwenywe alikuwa tayari kurudi lakini ilishindikana. Mkataba wa Toney na matajiri hawa wa Saudia unamalizika mwaka 2028.
Nicolas Jackson
MSHAMBULIAJI wa Chelsea ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Bayern Munich, Nicolas Jackson huenda akarejea katika viunga vya Stamford Bridge kwa muda kabla ya kutafuta sehemu nyingine yakwenda kwa msimu ujao.
Jackson mwenye umri wa miaka 24, ameshindwa kuonyesha kiwango bora akiwa na Bayern hali inayosababisha mabosi wa timu hiyo wasimpe mkataba wa moja kwa moja. Kwa mujibu wa taarifa Jackson haitaji kuichezea tena Chelsea.
Victor Osimhen
MABOSI wa Napoli waliweka kipengele katika makubaliano yao ya mauzo na Galatasaray juu ya mshambuliaji wao wa kimataifa wa Nigeria, Victor Osimhen ambacho kinaeleza ikiwa timu hiyo itahitaji kumuuza Osimhen kwenda timu ya Italia, itatakiwa kuilipa Napoli Pauni 60 milioni.
Osimhen mwenye umri wa miaka 27, ameendelea kuonyesha kiwango bora katika kikosi cha kwanza cha Galatasaray alichosaini nacho mkataba wa moja kwa moja katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Andrea Cambiaso
MANCHESTER City, Liverpool na Real Madrid zinadaiwa kuwa katika vita kali ya kuiwania saini ya beki wa pembeni wa Juventus na timu ya taifa ya Italia, Andrea Cambiaso mwenye umri wa miaka 26.
Mabosi wa Juventus hawaonekani kuwa tayari kumuuza staa huyu lakini mchezaji mwenyewe ameshawaambia anahitaji kuondoka kwani anaamini ni muda sahihi wa kufanya hivyo.