Barcelona, Real Madrid bado zinamhitaji Rodri
Muktasari:
- Taarifa zinaeleza kuwa klabu hizo mbili zinafahamu mchango mkubwa wa Rodri katika mafanikio ya Man City na licha ya majeraha ya mara kwa mara ambayo fundi huyu amekuwa akiyapata wanaamini bado atawasaidia sana.
MANCHESTER City inakabiliwa na presha kubwa ya kumbakisha kiungo wake wa kimataifa wa Hispania, Rodri, 29, kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi, baada ya vigogo wa La Liga, Real Madrid na Barcelona kuonyesha nia ya kumsajili.
Taarifa zinaeleza kuwa klabu hizo mbili zinafahamu mchango mkubwa wa Rodri katika mafanikio ya Man City na licha ya majeraha ya mara kwa mara ambayo fundi huyu amekuwa akiyapata wanaamini bado atawasaidia sana.
Hata hivyo, Man City haina mpango wa kumuuza kirahisi mchezaji huyu ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Licha ya ukweli kwamba Man City haitaki kumuuza, lakini ikiwa Rodri mwenyewe atalazimisha kuondoka kuna uwezekano wa matajiri hao wa Jiji la Manchester kumzuia.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Rodri amecheza mechi 22 za michuano yote na kufunga bao moja.
Endapo itaamua kumuuza, Man City inaweza kuhitaji takribani Pauni 100 milioni kama ada yake ya uhamisho kiasi ambacho kinaonekana kuwa kitaleta ugumu kwa Barcelona ambayo haipo sawa kiuchumi kwa sasa.
Zeki Celik
MATUMAINI ya Liverpool kumsajili beki wa AS Roma na timu ya taifa ya Uturuki, Zeki Celik, 29, yameongezeka, baada ya wakala wake kuweka wazi kwamba mchezaji huyo hataki kujiunga na Juventus.
Inaelezwa kuwa Liverpool inamwona Celik kama chaguo sahihi la kuongeza ushindani katika upande wa kulia wa safu yao ya ulinzi.
Uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya fundi huyu unatarajiwa kufanyika baada ya msimu kumalizika.
Julian Alvarez
ARSENAL na Chelsea zimejumuika pamoja na Barcelona katika mbio za kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Argentina Julian Alvarez, 26.
Taarifa zinaeleza kuwa klabu hizo mbili za Ligi Kuu England zinaamini Alvarez ana uwezo wa kuleta utofauti mkubwa katika safu zao za ushambuliaji, lakini ushindani wa kuiwania huduma yake umekuwa mkubwa.
Barcelona tayari imeshaanza mazungumzo, lakini ushindani wa kifedha kutoka kwa vigogo hao wa England unaweza kuwafanya Wahispania hao kufeli kumpata.
Guglielmo Vicario
JUVENTUS inamwangalia kipa wa Tottenham na timu ya taifa ya Italia, Guglielmo Vicario, 29, kama sehemu ya mipango yao ya muda mrefu na inataka kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Hata hivyo, dili hilo halitakuwa rahisi baada ya Inter Milan pia kuingia kwenye mbio za kumwania kipa huyo, ambaye ameonyesha kiwango bora tangu ajiunge na Spurs.
Inaelezwa kuwa Juventus ipo tayari kulipa zaidi ya Pauni 50 milioni kuhakikisha inaipata huduma ya fundi huyu.
Nick Woltemade
NEWCASTLE imesisitiza kuwa haitamuuza mshambuliaji wake wa kimataifa wa Ujerumani, Nick Woltemade (24) katika dirisha la majira ya kiangazi, labda mchezaji huyo mwenyewe aombe kuondoka.
Viongozi wa Newcastle United wanaamini Woltemade bado ni sehemu muhimu ya mipango yao ya baadaye na hawana presha ya kumtoa kwa sasa.
Hata hivyo, ikiwa staa huyo ataonyesha nia ya kuondoka, watakuwa tayari kusikiliza ofa zitakazowasilishwa.
Ivan Fresneda
ARSENAL imejitokeza kuwa kinara mbele ya Manchester City na Newcastle United katika mbio za kumsajili beki wa kulia wa Sporting CP na timu ya taifa ya Hispania Ivan Fresneda, 21.
Inaelezwa kuwa Arsenal imevutiwa na uwezo wake wa kucheza pande zote za ulinzi na mchango wake katika mashambulizi, jambo linalomfanya aendane na falsafa ya kocha Mikel Arteta.
Sporting inatarajiwa kuhitaji dau nono ili kumruhusu beki huyo chipukizi kuondoka, huku ushindani mkali ukitarajiwa kuendelea hadi mwisho wa dirisha la usajili.
Ben White
MABOSI wa Arsenal wanafikiria kuachana na beki wao Ben White katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi endapo itafanikiwa kumsajili beki wa Sporting CP, Ivan Fresneda katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Taarifa zinaeleza benchi la ufundi la Arsenal linaona kuwa ujio wa Fresneda utapunguza nafasi ya kucheza kwa Ben White kikosini, hasa ikizingatiwa ushindani uliopo katika safu ya ulinzi kwa sasa.
Ingawa White bado ni mchezaji muhimu, washika mitutu hao wapo tayari kusikiliza ofa kutoka timu zinazomhitaji.
Nathaniel Brown
MANCHESTER United na Arsenal zinadaiwa kuwa katika vita kali ya kuiwania saini ya beki kisiki wa Eintracht Frankfurt na timu ya taifa ya Ujerumani, Nathaniel Brown mwenye umri wa miaka 22.
Brown amekuwa akionyesha kiwango bora katika Bundesliga, hali iliyovutia macho ya vigogo wa Ligi Kuu England wanaotaka kuimarisha safu zao za ulinzi kwa msimu ujao.
Frankfurt inahitaji kiasi kikubwa cha pesa ili kumwachia staa huyo. Mkataba wa sasa wa Brown unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Trevoh Chalobah
CHELSEA ipo tayari kumruhusu beki wake wa kimataifa wa England, Trevoh Chalobah, 26, kujiunga na Aston Villa katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini kwa sharti la kupata mbadala wake kwanza.
Chalobah amekuwa akipata muda mchache wa kucheza katika kikosi cha kwanza cha Chelsea hali inayomfanya kutamani kuondoka.
Villa inaamini uzoefu wake wa EPL unaweza kuimarisha safu yao ya ulinzi kuelekea msimu ujao licha ya kwamba hapati nafasi ya kutosha kwa sasa.