Vigogo England wawasili Hispania dili la Gallagher
Muktasari:
- Kwa mujibu wa tovuti ya Sky Sports, miongoni mwa timu za England zinazomhitaji ni pamoja na Chelsea, Arsenal, Liverpool na Manchester City.
TIMU za Ligi Kuu England, zinaripotiwa kutuma wawakilishi kwenda Hispania kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Atletico Madrid kwa ajili ya kuipata saini ya kiungo wa kati wa timu hiyo na England, Conor Gallagher, katika dirisha lijalo la Januari.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sky Sports, miongoni mwa timu za England zinazomhitaji ni pamoja na Chelsea, Arsenal, Liverpool na Manchester City.
Gallagher ambaye awali alikuwa Chelsea kabla ya kutua Atletico anawindwa na vigogo kwa sababu ameonyesha nia ya kutaka kuondoka kwa kuwa amekuwa hapati muda mwingi wa kucheza.
Kiungo huyo ndiye mchezaji aliyetokea benchi mara nyingi zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote katika kikosi cha Atletico jambo ambalo halimfurahishi akiamini anastahili kuanza katika kikosi cha kwanza na siyo benchi.
Nafasi yake kwa sasa inaonekana kuchukuliwa na Pablo Barrios, 22, ambaye ni zao la akademi ya timu hiyo.
Baadhi ya timu zinaangalia ikiwa zinaweza kumchukua kwa mkopo wa miezi sita hadi dirisha kubwa la usajili lijalo na nyingine zipo tayari kutoa mkwanja ili kumnunua mchezaji huyo mwenye miaka 25.
Antoine Semenyo
LLIVERPOOL tayari imefanya mazungumzo kuhusu uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth na timu ya taifa ya Ghana, Antoine Semenyo, 25. Wababe hao wa Anfield wapo tayari kulipa Pauni 65 milioni zilizowekwa kwenye mkataba wa mchezaji huyo. Semenyo amekuwa akionyesha kiwango bora Ligi Kuu England tangu msimu uliopita na msimu huu amecheza mechi 12 za michuano yote na kufunga mabao sita.
Assan Ouedraogo
MANCHESTER United na Chelsea zinamfuatilia kwa karibu kiungo wa kati wa RB Leipzig na Ujerumani, Assan Ouedraogo, 19. Ouedraogo ambaye anatajwa kuwa hazina ya Ujerumani kwa siku za usoni, kwa mujibu wa Sky Sports anataka kuendelea kusalia Bundesliga hadi mwisho wa msimu huu ambapo anaamini atakuwa amekua zaidi. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2029.
Jean-Philippe Mateta
MABOSI wa AC Milan, inaandaa ofa kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Crystal Palace na Ufaransa, Jean-Philippe Mateta,28. Mateta amekuwa akifanya vizuri England na inaamini akitua katika kikosi chake atakwenda kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji. Awali, Man United ilikuwa ni miongoni mwa timu zilizotajwa kutaka kumsajili staa huyo.
Dayot Upamecano
PARIS St-Germain imeingia rasmi katika vita ya kuwania saini ya beki kisiki wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Dayot Upamecano, mwenye umri wa miaka 27, ambaye anatarajiwa kuwa huru mwishoni mwa msimu. Taarifa zinadai Upamecano amekataa kusaini mkataba mpya na amesisitiza kwamba anataka kuondoka kujaribu changamoto mpya sehemu nyingine.
Matt O’Riley
MARSEILLE ya Ufaransa inataka kuanza mazungumzo na Brighton kuhusu uwezekano wa kumsainisha mkataba wa moja moja kiungo wa kati wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Denmark, Matt O’Riley, mwenye umri wa 25, katika dirisha lijalo la majira ya baridi. Benchi la ufundi la Marseille limevutiwa na kiwango ambacho O’Riley amekionyesha tangu alijiunga kwa mkopo katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Bernardo Silva
STAA wa Man City na timu ya taifa ya Ureno, Bernardo Silva, 31, anataka kuachana na matajiri hao mwisho wa msimu ambapo mkataba wake utakuwa unamalizika. Silva ambaye amekuwa mchezaji muhimu Man City kwa zaidi ya miaka saba anaamini sasa ni wakati sahihi wa kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine. Kuna tetesi anaweza kutua Ureno au Saudi Arabia.
Joao Gomes
KIUNGO wa kati wa Wolves na Brazil, Joao Gomes, 24, amevutiwa na mpango uliowasilishwa na Manchester United ambayo inataka kumsajili, hivyo yupo tayari kutua ifikapo Januari mwakani. Baadhi ya taarifa zimefichua Wolves pia ipo tayari kumwachia lakini inahitaji zaidi ya Pauni 50 milioni. Mkataba wa Gomes unatarajiwa kumalizika 2030.