Victor Ikpeba: Achraf Hakimi amestahili tuzo ya Afrika
Muktasari:
- Ikpeba anaamini kuwa mchezaji huyo wa Morocco amestahili tuzo hiyo kutokana na mafanikio yake akiwa na klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa msimu uliopita 2024-2025.
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, Victor Ikpeba, ametaja sababu iliyomfanya beki wa Morocco, Achraf Hakimi, kutangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika 2025 (CAF Player of the Year 2025) mbele ya mshambuliaji wa Nigeria, Victor Osimhen.
Ikpeba anaamini kuwa mchezaji huyo wa Morocco amestahili tuzo hiyo kutokana na mafanikio yake akiwa na klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa msimu uliopita 2024-2025.
Beki huyo wa kulia mwenye miaka 27, alikuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo ya jijini Paris kilichotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League), Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), huku klabu yake ikifika hatua ya fainali kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Klabu (FIFA Club World Cup), wakafungwa na Chelsea.
Hakimi amewashinda Osimhen na mshambuliaji wa Misri, Mohamed Salah, katika kinyang’anyiro hicho, ambacho kiliwavutia mashabiki wengi wa soka barani Afrika.
Osimhen aliingia kwenye orodha ya waliochaguliwa kuwania tuzo hiyo, kufuatia kufunga mabao 37 na kutoa asisiti 8 katika mechi 41 akiwa Galatasaray, na kuisaidia klabu hiyo ya Uturuki kutwaa mataji mawili ya ndani.
Ikpeba anaamini kwamba Hakimi amestahili kutangazwa mshindi kutokana na mchango wake mkubwa katika timu ya PSG iliyoshinda mataji matatu makubwa (treble).
“Tunakatishwa tamaa kuwa hatutakwenda Kombe la Dunia, lakini Victor amekuwa bora sana kwa shauku na kujituma anapochezea timu ya taifa bila mipaka,” amesema.
“Kati ya wachezaji watatu, nafikiri Hakimi amekuwa bora, alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu ya Ufaransa, na kufika fainali Kombe la Dunia la Klabu. Lakini kwa uzuri wa soka, naamini kabisa kuwa yeye ndiye mshindi aliyestahili,” amesema Ikpeba.
Katika tuzo za CAF 2025 zilizotolewa jana Jumatano, Novemba 19, 2025, upande wa Wanawake, Ghizlane Chebbak wa Morocco alichaguliwa kuwa mchezaji Bora wa Afrika kutokana na mchango wake mkubwa kwenye timu ya taifa.
Katika nafasi za kipa, Yassine Bounou (Morocco) alichaguliwa kipa bora kwa wanaume, huku Chiamaka Nnadozie (Nigeria) akipata heshima hiyo kwa wanawake. Tuzo za wachezaji wadogo zilienda kwa Othmane Maamma (Morocco) kwa wanaume na Doha El Madani (Morocco) kwa wanawake.
Timu za taifa pia zilipewa heshima, ambapo Morocco U-20 ilichaguliwa kuwa timu bora ya taifa ya wanaume, na Nigeria ikipata heshima hiyo kwa upande wa wanawake.
Kwa klabu, Pyramids FC ya Misri ilitangazwa klabu bora ya Mwaka Wanauem, huku majina ya wachezaji na makocha wa mwaka yakiwemo Bubista wakitambuliwa kwa mafanikio yao.
Huu umekuwa mwaka wa Morocco katika soka la Afrika, kwani wachezaji wake walishinda tuzo nyingi na kuonyesha ubora mkubwa kwenye mashindano ya ndani na kimataifa.