VAR yaivurugia Benin AFCON 2025, yashindwa kufanya kazi
Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea dakika za mwisho za mechi hiyo, wakati Chancel Mbemba alipogusa mpira kwa mkono ndani ya eneo la hatari la DR Congo.
Mechi ya Kundi C katika Fainali za AFCON 2025 kati ya DR Congo na Benin, iliyochezwa leo Jumanne, Desemba 23, 2025 kwenye Uwanja wa Al Madina nchini Morocco, imebaki na mjadala mkubwa baada ya Benin kukosa fursa ya penalti kutokana na VAR kushindwa kufanya kazi.
Tukio hilo lilitokea dakika za mwisho za mechi hiyo, wakati Chancel Mbemba alipogusa mpira kwa mkono ndani ya eneo la hatari la DR Congo.
Kwa mujibu wa sheria za FIFA, tukio kama hilo lingepelekea penalti, lakini kwa kuwa VAR ilikuwa na tatizo la kiufundi kwa takriban dakika 10, mwamuzi hakutambua makosa hayo uwanjani. Hii ilisababisha Benin kushindwa kupata fursa ya kusawazisha, na matokeo ya mwisho kuibeba DR Congo iliyoshinda 1-0.
Kocha wa Benin na wachezaji wa kikosi hicho walionyesha kuchukizwa na tukio hilo, wakisema tatizo la teknolojia halipaswi kuwa kisingizio cha timu kushindwa kupata haki yake, huku mashabiki wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha mfumo wa VAR ili kuepuka matatizo kama hayo katika mashindano makubwa ya kimataifa kama AFCON.
Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu utekelezaji wa teknolojia ya VAR barani Afrika na umuhimu wa kuhakikisha haina hitilafu wakati wa mechi muhimu.
DR Congo, licha ya changamoto hiyo, imeendelea kuongoza Kundi C ikiwa na pointi 3, huku Benin ikibakia bila pointi na ikijipanga upya kwa mechi zijazo.