VAR: Kwanini bao la Ecuador vs Qatar lilikataliwa kirahisi namna ile?

PATASHIKA ya Kombe la Dunia ilianza juzi ambapo wenyeji Qatar walioneshana kazi na Ecuador katika mchezo wa kundi A.

Mchezo huo uliambatana na shamrashamra za ufunguzi wa mashindano hayo ambayo uwekezaji wake ni wa kihistoria.

Katika uwekezaji wake Qatar imejenga viwanja saba vipya ambapo uwanja wa nane ni wa zamani ambao umefanyiwa ukarabati wa hali ya juu. Katika ujenzi wa viwanja Qatar imewekeza Dola 300 bilioni na kuzipiku nchi nyingi zilizowahi kuandaa fainali hizo.

Ikumbukwe kuwa ni miaka 12 sasa tangu Qatar ipewe haki ya kuandaa mashindano hayo. Ni mashindano ambayo yanavuta hisia za mashabiki wengi wa soka duniani na naweza kusema ‘mtoto hatumwi dukani’, huku ugomvi wa rimoti za runinga ukiongezeka kwani kuna baadhi watataka kuangalia tamthilia pendwa huku wengine wakipendelea ‘boli’.

Pia ni mashindano ambayo Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) linatarajia kuvuna zaidi ya Dola 4.7 billioni kutokana zabuni kadhaa kwa ajili ya michuano hiyo.

Katika haki ya matangazo ya televisheni Fifa itavuna Dola 2.64 bilioni huku haki ya masoko ikiingiza Dola 1.35 bilioni ilhali mauzo ya tiketi yakiingiza Dola 500 bilioni.

Ni mashindano ambayo yanafanyika kwenye ardhi ya Mashariki ya Kati kwa miaka 92 ya kihistoria tangu kuanzihishwa kwake na kuwa mashindano ya kwanza kufanyika katika eneo hilo.

Pia ni mashindano ya kwanza ya Fifa kufanyika Novemba na Desemba tofauti na miaka ya nyuma ambapo yalikuwa yanafanyika katikati ya mwaka.

Fifa ilikubaliana na ombi la Qatar ili kukwepa kipindi kigumu cha kiangazi na kusababisha kuahirishwa kwa ligi mbalimbali za Ulaya kinyume na ilivyozoeleka.

Pilikapilika za michuano hiyo zitaendelea leo ikiwa ni siku ya tatu ambapo Argentina chini ya nyota wa PSG, Lionel Messi itapepetana na Saudi Arabia kuanzia saa 7.00 mchana wakati saa 10 katika mchezo wa kundi C, ambapo kundi D kutakuwa na mechi kati ya Denmark dhidi ya Tunisia kuanzia saa 10.00 jioni.

Mchezo mwingine wa kundi C utakuwa baina ya Mexico dhidi ya Poland ambao umepangwa kuanza saa 1.00 usiku wakati kuanzia saa 4.00 usiku Ufaransa chini ya Kylian Mbape itachuana na Australia.

Ni michuano ambayo msisimko wake ni mkubwa kupindukia pamoja na kuwepo kwa malalamiko kadhaa kutoka kwa baadhi ya mataifa ya Ulaya dhidi ya Fifa na waandaaji ambayo naweza kusema hayana mashiko kwani mashabiki wa soka wamejipanga kwa ajili ya kupata burudani ya soka na si vinginevyo. Baada ya kuwapa taarifa hiyo kuhusiana na uwekezaji na ratiba ya mashindano, sasa turejee katika mada husika ya VAR.

Katika toleo lililopita tulizungumzia teknolojia ya kisasa ya kung’amua kuzidi au kwa king’eng’e inajulikana kwa jina la Semi-Automated Offside Technology (SAOT) ambayo kwa mara ya kwanza ilitumika katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi ikiwa katika dakika ya tatu tu. Furaha ya wachezaji na mashabiki wa timu ya Ecuador ilizimwa mapema zaidi baada ya bao lao lililofungwa na mchezaji wa zamani wa klabu za West Ham United na Everton, Enner Valencia kuingia katika mfumo wa SAOT. Valencia alifunga bao hilo kwa kichwa akitumia vyema mpira wa kurushwa wa Felix Torres. Wachezaji wa Ecuador walishangilia bao hilo huku wenzao wa Qatar wakirejea kwa unyonge kutokana na bao hilo. Lakini, dakika chache baada ya mpira wa kichwa wa Valencia kuingia wavuni, mwamuzi kutoka Italia, Daniele Orsato alionyesha kwamba bao hilo halipaswi kutekelezwa baada ya ukaguzi wa VAR.


KWANINI GOLI LILIKATALIWA NA VAR?

Bao la ufunguzi lilikataliwa baada ya mchezaji Pervis Estupinan kurusha mpira wa adhabu ndani ya eneo la hatari. Kiatu cha kulia cha Michael Estrada kilikuwa katika eneo la kuotea baada ya mpira kutoka kwa Felix Torres, ambaye alikuwa akimpinga kipa wa Qatar, Saad Al Sheeb.

Estrada alirudisha mpira huo kwa Torres ambaye alicheza boli ya sarakasi kwa Valencia ambaye alifunga.

Uamuzi huo ulihusisha matumizi ya teknolojia ya SAOT ambayo imeanza kutumika rasmi katika mashindano haya pamoja na uwepo wa VAR na mwamuzi wa ndani ya uwanja akisimamia sheria 17 za soka.


KWA WASOMAJI

Teknolojia ya SAOT huanza kufanya kazi katika mfano wakati bao limefungwa au uamuzi unaoweza kubainisha matokeo umefanywa (penalti au kadi nyekundu).

Teknolojia hiyo inatumia kamera 12 ambazo zote zinafuatilia mpira na kuweza kupata matukio 29 ya kila mchezaji kwa muda mfupi (wakati wa tukio limefanyika) na kutoa uamuzi wa haraka zaidi. Matukio au pointi hizo 29 za data ni pamoja na viungo na sehemu zote za mwili ambazo zinafaa kufanyia uamuzi wa kuotea au kuzidi kwa mujibu wa sheria hiyo namba 11 ya soka duniani ambayo mpaka sasa ina ukakasi mkubwa katika kutoa uamuzi.

Kitengo cha kipimo kisicho na usawa kitawekwa eneo la ndani ya katikati ya mpira na itatuma data kwenye chumba cha operesheni ya video mara 500 kwa sekunde ambayo itaruhusu kutambua kwa usahihi wakati mpira umepigwa. Mara tu mchezaji anapopokea mpira katika nafasi ya kuotea teknolojia hutoa tahadhari moja kwa moja kwa maofisa katika chumba maalumu cha kufanyia kazi na baada ya kupata uamuzi ndipo mwamuzi hupewa taarifa baada ya uamuzi huo kupitishwa.

Suala la kutoa uamuzi huwa sekunde, ingawa uamuzi katika mechi hiyo ya ufunguzi wa Kombe la Dunia la 2022 ulichukua muda mrefu zaidi.