Van Dijk: Bado tunataka straika
Muktasari:
- Lakini, kauli hiyo ya Van Dijk inaonekana kukinzana na ya kocha Arne Slot.
LIVERPOOL, ENGLAND: NAHODHA wa Liverpool, beki wa kati Virgil van Dijk amesema timu hiyo ya Anfield bado ina tatizo kwenye safu yake ya ushambuliaji, inahitaji straika mpya baada ya kuchapwa na Crystal Palance kwenye Ngao ya Jamii.
Lakini, kauli hiyo ya Van Dijk inaonekana kukinzana na ya kocha Arne Slot.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England walichapwa kwa penalti katika mechi ya Ngao ya Jamii uwanjani Wembley, Jumapili.
Straika mpya, Hugo Ekitike, aliyenaswa kwa Pauni 79 milioni alionyesha kiwango bora, akifunga dakika ya nne tu ya mchezo wake wa kwanza wa ushindani tangu alipojiunga akitokea Eintracht Frankfurt, huku akiwa na muunganiko bora kabisa na staa mwingine mpya, Florian Wirtz.
Lakini, Liverpool ilionekana kuwa na tatizo kwenye safu ya ulinzi na Van Dijk alifanya makosa mawili, kwanza alisababisha penalti na kisha akiacha nafasi nyuma kufanya mechi hiyo kumalizika kwa matokeo ya 2-2 kabla ya kufikia kwenye kupigiana mikwaju ya penalti.
Liverpool wikiendi iliyomalizika ilimpiga bei Darwin Nunez kwenda Saudi Arabia kujiunga na Al Hilal, huku ikiwa ishampiga bei Luis Diaz kwenda Bayern Munich na imempoteza mshambuliaji wao Diogo Jota, aliyefariki dunia kwenye ajali ya gari huko Hispania na kuzikwa Ureno.
Hakuna kificho straika Alexander Isak yupo kwenye rada za mabosi wa Liverpool, lakini Newcastle United ilishagomea ofa ya Pauni 110 milioni ya kumhusu mshambuliaji huyo baada ya wababe hao wa Anfield kumtaka.
Isak, kwa sasa amewekwa kando kwenye mazoezi ya Newcastle, huku mwenyewe akilazimisha uhamisho wa kwenda kujiunga na Liverpool.
Wakati Ekitike na Wirtz wakionyesha kiwango bora, washambuliaji Mohamed Salah na Cody Gakpo, nao walianzishwa kwenye mechi hiyo, ambayo nahodha na beki wa kati, Van Dijk anadai timu ina tatizo kwenye sehemu ya fowadi.
"Tumempoteza Darwin, amekwenda Saudia na tumempoteza Lucho, amekwenda Bayern,” alisena Van Dijk na kuongeza. “Nadhani kuna nafasi kwenye eneo la straika ili kuongeza nguvu na dirisha hili linahitaji kuboresha timu iwe sawa."