Uzi wa taifa lako Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Na Argentina itakwenda kwenye fainali hizo ikiwa na kazi ya kutetea ubingwa ikiwa na jezi za mtindo uleule ambazo ziliwafanya wanyakua taji hilo mwaka 1978, 1986 na 2022.
LONDON, ENGLAND: UJERUMANI itarudisha kumbukumbu ya nyuma kabisa kufuatia jezi itakazovaa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya Adidas kutambulisha uzi wa nyumbani utakaotumiwa na mataifa 22 katika michuano hiyo itakayofanyika huko Marekani, Canada na Mexico.
Na Argentina itakwenda kwenye fainali hizo ikiwa na kazi ya kutetea ubingwa ikiwa na jezi za mtindo uleule ambazo ziliwafanya wanyakua taji hilo mwaka 1978, 1986 na 2022.
Ingawa kwamba Ujerumani bado haijafuzu kwa fainali hizo za Kombe la Dunia 2026, Argentina yenyewe imeshaweka kibindoni tiketi yao mapema ikiungana na England, ambayo imeshafuzu.
Adidas imefanya utambulisha wa jezi zake zitakazotumiwa na timu zitakazopambana kwenye kusaka ubingwa huo wa dunia, huku kampuni hiyo ya vifaa vya michezo ikiwa na idadi kubwa ya timu inayozivika kwenye fainali hizo.
Kwa jezi hizo za Ujerumani zimenogeshwa na michoro ya dizaini zilizopita, ikiwamo mtindo ule wa jezi walizovaa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2014 zilizofanyika Brazil, ambapo walifanikiwa kunyakua ubingwa. Hiyo itakuwa mara yao ya mwisho kuvaa jezi za adidas kabla ya kuhamia kwenye dizaini za Nike kuanzia 2027, hivyo jambo hilo litafikisha mwisho miaka 70 ya adidas kuitengenezea jezi timu ya taifa ya Ujerumani.
Straika wa Newcastle United, Nick Woltemade na kiungo mchezeshaji wa Liverpool, Florian Wirtz ni miongoni mwa mastaa wa Ujerumani waliotumika kwenye utambulisho wa jezi hizo.
Argentina itakwenda kupambana kutetea taji hilo kwenye jezi zake za michirizi ya mistaari ya bluu bahari na miupe, huku ikiwa na maandishi ya namba 1896 yaliyowekwa upande wa nyuma wa shingo ikielezea mwaka ulionzishwa chama cha soka cha nchi hiyo.
Jezi hizo zimetengenezwa kwa kuzingatia hali ya hewa ya nchi za Marekani, Canada na Mexico, ambako zitafanyika fainali hizo za Kombe la Dunia.
Nchi nyingine zilizotengenezewa jezi zao za nyumbani ambazo zitafaa kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia 2026 ni Scotland, Wales na Northern Ireland, ambazo bado zinapambana kukamatia tiketu. Adidas pia imetambulisha jezi za Algeria, Ubelgiji, Chile, Colombia, Costa Rica, Hungary, Italia, Japan, Mexico, Peru, Qatar, Saudi Arabia, Hispania, Sweden, Ukraine, United Arab Emirates na Venezuela.
Thomas Mace, makamu wa rais wa dizaina wa Adidas Football alisema jezi hizo zimetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu ambayo itamfanya mchezaji kuwa mkavu na kucheza soka lake kwa uhuru mkubwa katika fainali hizo hata kama kutakuwa na joto la kiwango cha juu.
Jezi hizo zilianza kuingizwa sokoni, Alhamisi, Novemba 7 kwa ajili ya kuanza kuuzwa.