Usipojipanga, utapangwa EPL

LONDON, ENGLAND. KUSHINDA taji la nne mfululizo kwenye Ligi Kuu England, Manchester City haitakubali kuangusha pointi yoyote dhidi ya wapinzani wake kwenye mchakamchaka wa ligi hiyo, wakati kesho, Jumapili itakapokuwa Etihad kukipiga na vinara, Arsenal.

Mabingwa hao watetezi bado hawajapata ushindi kwenye mechi yoyote dhidi ya timu tano za juu katika msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu.

Ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Arsenal na Aston Villa na iliambulia sare dhidi ya Liverpool (mara mbili) na Tottenham Hotspur.

Wakati ikitarajia kuikaribisha Arsenal huko Etihad, mechi hiyo kwa Man City si tu ya lazima kushinda, bali kujiondoa kwenye tatizo hilo la kushindwa kuzichapa timu zilizopo nafasi za juu kwenye msimamo.

Rekodi zinaonyesha kwamba Man City na Arsenal zimekutana mara 53 kwenye Ligi Kuu England, ambapo The Gunners imeshinda 24 na mara 13 ni kwenye Uwanja wa Emirates na mechi 11 ilishinda Etihad.

Miamba hiyo imetoka sare mara 10, huku Man City ikishinda 19, mara 12 uwanjani Etihad na saba Emirates. Mechi tano za mwisho walizokutana kwenye ligi, Man City imeshinda nne, Arsenal moja, ambayo ni ile iliyopita kwenye mzunguko wa kwanza msimu huu.

Utamu wa wikiendi hii kwenye Ligi Kuu England ni kwamba timu zote zitazoshindania ubingwa wa msimu huu zitakuwa uwanjani kesho, Jumapili.

Ukiweka kando kipute cha Man City na Arsenal, mpinzani wao kwenye mbio za ubingwa, Liverpool wenyewe watatangulia kwa kipute cha kibabe watakapokipiga na Brighton huko Anfield.

Ushindi wa vijana wa Jurgen Klopp mbele ya Roberto De Zerbi utawafanya kushika usukani wa ligi hiyo, kisha wakaomba sare tu kwenye kipute cha Etihad.

Namba zinaonyesha kwamba Liverpool la Brighton zimekutana mara 13 kwenye Ligi Kuu England, ambapo ukiondoa mechi nne zilizomalizika kwa sare, Liverpool imeshinda saba  - tatu ikiwa nyumbani na nne ugenini, wakati Brifhton imeshinda mbili, nyumbani moja na nyingine ugenini.

Rekodi ya mechi zao tano zilizopita walizokutana wenyewe, Liverpool imeshinda moja, Brighton moja huku mechi tatu zikimalizika kwa sare.

Hata hivyo, mchakamchaka wa Ligi Kuu England utaanza leo Jumamosi baada ya kusubiri kwa wiki mbili kupisha mikikimikiki ya mechi za kimataifa.

Kasheshe litaanzia huko St James’ Park, ambapo Newcastle United itakuwa nyumbani kukipiga na West Ham United ya kocha David Moyes.

Newcastle United na West Ham United zimekutana mara 51 kwenye mechi za Ligi Kuu England, ambapo mara 14 zilitoka sare, huku West Ham ikishinda 14, mara tisa nyumbani na tano ugenini, huku Newcastle imeshinda 23, mara 12 nyumbani na 11 ilipocheza ugenini.

Kwenye mechi tano zilizopita, Newcastle imeshinda moja na West Ham moja, huku mechi tatu zikiisha kwa sare. Hilo linathibitisha ubabe uliopo miamba hiyo inapokutana. Lazima pachimbike.

Kipute kingine chenye upinzani wa kutosha kitakuwa huko Vitality Stadium, ambapo Bournemouth itakuwa nyumbani kuikaribisha Everton. Miamba hiyo imekutana mara 13 kwenye mechi za Ligi Kuu England, ambapo Bournemouth imeshinda tano, nne nyumbani na moja ugenini, wakati Everton imeshinda sita, huku mara zote ilizoshinda ilifanya hivyo kwenye Uwanja wa Goodison Park, ikiwa haijawahi kushinda ugenini, mahali ambako utafanyika mchezo wa leo. Mechi baina yao ziliisha kwa sare, huku mechi tano za mwisho, Everton imeshinda mbili na Bournemouth tatu.Moto mwingine utawaka huko Stamford Bridge, ambapo Chelsea itashuka uwanjani kujitafuta mbele ya Burnley, inayopambana kuhakikisha inabaki kwenye Ligi Kuu England.

Chelsea inatafuta namna ya kupata ushindi ili kupata tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao. Rekodi zinawabeba, ambapo kwenye mechi 17 walizokutana na Burnley kwenye Ligi Kuu England, imeshinda 12, nne nyumbani na nane ugenini, wakati Burnley imeshinda moja, ilipocheza ugenini. Mechi nne zilimalizika kwa sare. Kwenye mechi tano zilizopita walizokutana, Chelsea imeshinda nne na moja tu ilimalizika kwa sare.

Ngoja tuone safari hii itakuwaje, Chelsea itaandikisha ushindi wake wa tano nyumbani, au Burnley itashinda kwa mara ya pili Stamford Bridge.

Kutakuwa na vita ya kukwepa kushuka daraja huko The City Ground, wakati Nottingham Forest itakapokipiga na Crystal Palace. Rekodi zinaonyesha kwamba Palace ni kibonde kwa Forest, ambapo katika mechi tano za mwisho walizokutana, sare mbili na Forest imeshinda tatu. Lakini, miamba hiyo kwa ujumla wake kwenye Ligi Kuu England zimekutana mara saba, nne  zilimalizika kwa sare, huku Forest ikishinda tatu, mbili nyumbani na moja ugenini na Palace haijawahi kupata ushindi wowote mbele ya Forest kwenye ligi. Sheffield United itajimwaga kwenye uwanja wa nyumbani wa Bramall Lane kukipiga na Fulham katika mechi nyingine ya kibabe kabisa kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England. Mechi tano ilizokutanisha timu hizo kwenye Ligi Kuu England, Sheffield United imeshinda moja tu, ilipocheza uwanjani Bramall Lane, wakati Fulham imeshinda tatu, zote nyumbani na mechi moja ilimalizika kwa sare. Mechi tano zilizopita, Fulham imeshinda tatu, sare moja na Sheffield United imeshinda moja.

Kwenye vita ya kusaka Top Four, Tottenham Hotspur itarusha kete yake muhimu kwenye vita hiyo, wakati itakapokuwa nyumbani kukipiga na Luton Town. Rekodi zinaonyesha, Spurs na Luton zimekutana mara moja tu, ambapo Spurs ilishinda, mechi iliyofanyika ugenini kwenye uwanja wa Luton na sasa itarudi kwenye uwanja wake wa nyumbani kujaribu kuzoa pointi tatu muhimu za kuwaweka vizuri kwenye vita ya kusaka Top Four.

Wapinzani wengine kwenye mbio za Top Four ni Aston Villa, ambao watakuwa Villa Park kukipiga na Wolves. Si mechi rahisi, ambapo kwenye mechi 17 ilizokutanisha miamba hiyo kwenye Ligi Kuu England, Aston Villa imeshinda tano na Wolves sita, huku mechi sita zilimalizika kwa sare.

Kwenye ushindi wa mechi za Aston Villa, ilifanya hivyo mara moja nyumbani na nne ugenini, huku Wolves imeshinda tatu nyumbani na tatu ugenini, kitu kinachofanya Villa Park patarajie vita ya kutisha.

Manchester United inayofukuzia nafasi ya kuwamo kwenye Top Four, ikiombea mabaya kwa Spurs na Aston Villa, yenyewe itakuwa ugenini Gtech Community kukipiga na Brentford ya straika Ivan Toney. Kwenye mechi tano ambazo Man United ilikutana na Brentford kwenye Ligi Kuu England, hakuna sare, Brentford imeshinda moja na Man United imeshinda nne, tatu nyumbani na moja ugenini. Kipute hicho cha leo kitakuwa na upinzani mkali, ambapo Brentford itasaka ushindi wake wa pili nyumbani dhidi ya Man United, ambao pia watahitaji kushinda mara ya pili ugenini dhidi ya wapinzani wao hao. Mechi tano zilizopita, Man United imeshinda nne, Brentford imeshinda moja, lakini kilikuwa kipigo kizito kwa Mashetani Wekundu, mabao 4-0.