Upamecano apewa ofa nono Bayern Munich
Muktasari:
- Upamecano amekuwa mhimili muhimu katika safu ya ulinzi ya mabingwa hao wa Ujerumani lakini mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
BEKI wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Dayot Upamecano, 27, yupo tayari kusaini mkataba mpya na Bayern ambao utamfanya abaki hadi Juni 2030.
Upamecano amekuwa mhimili muhimu katika safu ya ulinzi ya mabingwa hao wa Ujerumani lakini mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Katika dirisha lililopita la majira ya baridi alidaiwa kwa huenda angejiunga na Liverpool au Real Madrid ambazo zimekuwa zikimfuatilia kwa muda mrefu na zimezidisha juhudi hivi karibuni baada ya kuona mkataba wake unaelekea ukingoni.
Liverpool inahitaji sana huduma ya Upamecano kwa sababu wanamwona kama mbadala wa Ibrahim Konate ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika mwisho wa msimu huu na kuna uwezekano mkubwa akaondoka.
Kwa upande wa Madrid ambayo kwa sasa inapitia wakati mgumu, imekuwa ikimwinda Upamecano kwa sababu inaamini anaweza kwenda kuboresha safu yao ya ulinzi kutokana na uwezo wake.
Bayern inataka kumpa mkataba mpya pamoja na nyongeza ya mshahara ambao utafikia Euro 300,000 kwa wiki kutoka Euro 200,000 kwa wiki anaoupata kwa sasa.
Elliot Anderson
MANCHESTER United imemweka juu katika orodha ya wachezaji inaohitaji, kiungo wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya England, Elliot Anderson, 23, ili kuimarisha safu yao ya kiungo.
Mbali na Anderson, Man United pia inawafuatilia viungo wengine wawili ambao pia ni staa wa timu ya taifa ya England, Adam Wharton, 21, anayeichezea Crystal Palace, pamoja na Carlos Baleba, 22, wa Brighton na timu ya taifa ya Cameroon.
Inaripotiwa benchi la ufundi la Man United linataka kiungo mwenye nguvu, kasi na uwezo wa kuchezesha timu ili kuendana na mpango wao wa msimu ujao.
Cristian Romero
ATLETICO Madrid ipo tayari kuanza mazungumzo ya kumsajili beki wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Argentina, Cristian Romero, 27.
Hatua hiyo inakuja baada ya Romero kuchapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii unaodaiwa kuikosoa klabu yake, jambo lililozua tetesi kwamba anaweza kuwa tayari kuondoka Spurs.
Atletico ilitamani kumsajili Romero tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini ilishindikana kwa sababu mchezaji mwenyewe hakuwa anaonyesha nia ya kutaka kuondoka.
Sandro Tonali
MTENDAJI mkuu wa Newcastle United, David Hopkinson, amesema hana taarifa zozote kuhusu madai kwamba wakala wa kiungo wao Sandro Tonali, 25, alikuwa katika mazungumzo na Arsenal siku ya mwisho ya dirisha la usajili ili staa huyo ajiunge nao.
Kauli hiyo inakuja baada ya uvumi kuenea ukimhusisha kiungo huyo wa kimataifa wa Italia na uwezekano wa kujiunga na Arsenal katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya dili kudaiwa kufeli katika dirisha lililopita.
Tonali ameendelea kuwa sehemu muhimu ya mipango ya Newcastle, huku klabu hiyo ikisisitiza kwamba haijapokea ofa wala kufanya mawasiliano na timu yoyote.
Ruben Neves
KIUNGO wa kimataifa wa Ureno, Ruben Neves, 28, ameongeza mkataba wake wa kuendelea kusalia Al-Hilal ya Saudi Arabia hadi Juni 2029 baada ya uvumi kwamba huenda angeondoka katika dirisha lililopita la majira ya baridi.
Neves alikuwa akihusishwa na uwezekano wa kurejea barani Ulaya Januari, ambapo klabu kama Manchester United na Real Madrid ziliripotiwa kutamani kuipata huduma yake.
Hata hivyo, Hilal bado ilihitaji kuendelea kusalia na fundi huyo kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu ajiunge nao.
Robin Roefs
CHELSEA, Manchester City na Liverpool zimeingia kwenye mbio za kuwania saini ya kipa wa Sunderland na timu ya taifa ya Uholanzi, Robin Roefs, 23.
Inaripotiwa kuwa Sunderland wanatarajia kupokea ofa zitakazozidi Pauni 50 milioni kwa kipa huyo ambaye amekuwa katika kiwango bora na kuvutia klabu kubwa za Ulaya.
Roefs anaonekana kama uwekezaji wa muda mrefu kutokana na umri wake, uwezo wa kuokoa mipira migumu na uimara wake katika mechi kubwa, hali inayoongeza ushindani wa kumpata.
Casemiro
LA Galaxy kutoka Ligi Kuu ya Marekani (MLS) inaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa kimataifa wa Brazil, Casemiro, 33, anayetarajiwa kuondoka Manchester United mwishoni mwa msimu huu.
Casemiro alitangaza kuondoka mapema wiki iliyopita ikielezwa kuwa anahitaji kupata changamoto mpya sehemu nyingine baada ya kuitumikia timu hiyo tangu mwaka 2022.
Iwapo dili hilo litafanikiwa, staa huyo wa zamani wa Real Madrid atakuwa miongoni mwa mastaa wakubwa kujiunga na soka la Marekani ingawa pia kuna tetesi zinazomhusisha na Al Nassr ya Saudi Arabia.
Jhon Arias
WOLVES imekubali ofa ya Pauni 21.6 milioni kutoka klabu ya Brazil, Palmeiras, kwa ajili ya kumuuza winga wao wa kimataifa wa Colombia, Jhon Arias, 28. Arias tayari yupo kwenye mazungumzo ya maslahi binafsi na klabu hiyo ya Brazil, kwa ajili ya kukamilisha dili hilo.
Uhamisho huu unatarajiwa kukamilika ndani ya siku zijazo. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.