Unaijua Arsenal ya Afcon wewe?
Muktasari:
- Timu hiyo iliyodhaniwa kuwa ndogo imepangwa kukutana na vigogo Senegal kwenye mechi kubwa ya hatua ya 16 bora itakayochezwa Jumamosi hii.
CASABLANCA, MOROCCO: MASHABIKI wa soka huko kwenye mashindano ya Afcon 2025 wameibatiza Sudan jina la utani la “Arsenal ya AFCON” baada ya kuwa timu ya kwanza kabisa katika historia ya Kombe la Mataifa ya Afrika kufuzu hatua ya mtoano bila kufunga bao lolote.
Timu hiyo iliyodhaniwa kuwa ndogo imepangwa kukutana na vigogo Senegal kwenye mechi kubwa ya hatua ya 16 bora itakayochezwa Jumamosi hii.
Sudan walipata jina hilo la “Arsenal ya AFCON” kutokana na safari yao ya kushangaza.
Hii ni baada ya kumaliza kama moja ya timu bora zilizoshika nafasi ya tatu katika hatua ya makundi.
Hata hivyo, Sudan hawajafunga bao lolote la wazi katika michezo yao ya makundi, lakini kwa kushangaza waliweza kufuzu kwenda hatua ya mtoano.
Sudan walishinda mechi moja tu kati ya tatu za makundi, wakiifunga Equatorial Guinea kwa bao 1-0, huku ikipoteza 3-0 dhidi ya Algeria na 2-0 dhidi ya Burkina Faso.
Cha kushangaza zaidi, ushindi wao pekee ulitokana na bao la kujifunga la mchezaji wa Equatorial Guinea, Saul Coco na kukusanya pointi tatu zilizowavusha na kuingia mtoano.
Licha ya hilo, bao hilo la kujifunga, pointi tatu walizopata na tofauti ya mabao hasi manne (-4) ilitosha kabisa kuwapeleka Sudan hatua inayofuata. Hii iliweka historia mpya AFCON, kwani ilikuwa mara ya kwanza timu kufuzu kutoka makundi bila kufunga bao lolote wao yenyewe.
Mashabiki wenye mzaha hawakusita kuwalinganisha Sudan na vinara wa Ligi Kuu England, Arsenal. Arsenal wamekuwa katika kiwango bora msimu huu na wanaongoza Manchester City katika mbio za ubingwa.
Hata hivyo, kabla ya ushindi wao wa 4-1 dhidi ya Aston Villa Jumanne, mabao manne kati ya matano ya mwisho ya Arsenal uwanjani Emirates yalitokana na wapinzani kujifunga.
Mashabiki walichukua fursa hiyo kufanya utani kuhusu hali hiyo.
Mmoja amesema: “Arsenal ya AFCON.”
Mwingine akaandika: “Own Goal FC.”
Mwingine aliongeza: “Lakini wamefuzu kwenda hatua inayofuata.”
Huku mwingine akahitimisha: “Mafanikio ya ajabu na ya kihistoria kwa Sudan.”