Ule mpira wa Bao la Mkono wa Mungu unapigwa mnada

NEW YORK, MAREKANI. UNAMPENDA Diego Maradona? Unataka kubaki na kumbukumbu zake? Basi mchongo ni huu hapa, ule mpira uliotumika wakati anafunga Bao la Mkono wa Mungu, upo sokoni unapigwa mnada. Changamkia.

Gwiji huyo wa Argentina, jezi yake aliyovaa kwenye mechi hiyo ya robo fainali ya Kombe la Dunia 1986 wakati alipofunga mara mbili kuwachapa England 2-1, ilipigwa mnada Mei mwaka jana na kuuzwa Pauni 7 milioni. Ndiyo Pauni 7 milioni, zaidi ya Sh 20 bilioni za Kitanzania.

Na sasa mpira uliochezewa kwenye mechi hiyo unauzwa huko Marekani na mnada wake utafanyika Februari 8 baada ya kushindwa kuuzwa huko London kwa miezi miwili, licha ya kuwapo na ofa ya Pauni 2 milioni.

Mpira huo ambao ulikuwa kwa mwamuzi wa mchezo huo, Ali Bin Nasser, bei yake ya mnada itaanzia Pauni 485,000. Diego Maradona, ambaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 60 miaka miwili iliyopita, alifunga kwa mkono bao la kuongoza huko Mexico City. Aliruka juu, kisha akakunja mkono kugonga mpira kumpita kipa wa England, Peter Shilton - ambaye alikuwa na nafasi nzuri ya kudaka mpira, kama Diego angepiga kwa kichwa.

Shilton hajawahi kumsamehe Maradona - ambaye baadaye alipiga chenga wachezaji kibao wa England na kufunga bao la pili matata kabisa kuifanya Argentina kuwa mbele kwa mabao 2-0.

Gary Lineker aliifungia Three Lions bao la kujifariji, huku Argentina walisonga mbele na kumchapa Ujerumani Magharibi 3-2 kwenye mchezo wa fainali. Mpira huo wa adidas kwa sasa hauna upepo - ulikabidhiwa kwa refa wa mchezo, Bin Nasser siku ya Juni 22, 1986.Lakini, kwa sasa utawekwa kwenye mnada na kampuni ya Goldin.