Ulaya kwa motooo! Arsenal na Chelsea

Muktasari:
- Huko England kipute matata ni kile cha Arsenal na Chelsea uwanjani Emirates, wakati Hispania balaa litakuwa Wanda Metrolitano pale Atletico Madrid itakapokipiga na Barcelona
LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu za Ulaya ni mchakamchaka chinja. Si Ligi Kuu England, La Liga, Bundesliga, Serie A wala Ligue 1 kwenye afadhali, kote ni moto.
Huko England kipute matata ni kile cha Arsenal na Chelsea uwanjani Emirates, wakati Hispania balaa litakuwa Wanda Metrolitano pale Atletico Madrid itakapokipiga na Barcelona, huku Italia kasheshe ni la Atalanta na Inter Milan na Ufaransa, Paris Saint-Germain itaonyeshana ubabe na Marseille. Mechi hizo ni Jumapili.
Kwenye La Liga, Sevilla itacheza na Athletic Bilbao, Osasuna na Getafe na Real Vallecano itakipiga na Real Sociedad, wakati kwenye Bundesliga, burudani itakuwa baina ya VfL Bochum na Eintracht Frankfurt, FC Heidenheim itakipiga na Holstein Kiel na VfB Stuttgart itamaliza ubishi na vijana wa Xabi Alonso, Bayer Leverkusen.
Huko Serie A, Napoli itakuwa ugenini kucheza na Venezia, huku Bologna ikikipiga na Lazio, AS Roma na Cagliari na Juventus itaifuata Fiorentina kwao. Kwenye Ligue 1, mechi za Jumapili, Lyon itakuwa nyumbani kukipiga na Le Havre, huku Brest ikiwa na kasheshe mbele ya Reims, Montpellier na Saint-Etienne na Strasbourg na Toulouse.
Kimbembe kinaanzia Jumamosi, ambapo kwenye Ligi Kuu England shida itakuwa huko Etihad, wakati Manchester City itakapocheza na Brighton, Ipswich Town itakipiga na Nottingham Forest, Southampton na Wolves, wakati Everton ya David Moyes itacheza na West Ham United na Bournemouth itamaliza ubishi na Brentford.
Kwenye La Liga kutakuwa na mechi nne, ambapo Villarreal watakuwa nyumbani kumkaribisha Vinicius Jr na jeshi lake la Real Madrid, wakati Girona na Valencia zitakuwa kwenye kasheshe zito kama ilivyo kwa Mallorca na Espanyol na Real Valladolid na Celta Vigo.
Bundesliga moto utawaka wakati Augsburg itakapokipiga na Wolfsburg, Mainz 05 na Freiburg, Union Berlin na Bayern Munich, huku Werder Bremen ikiwa nyumbani kucheza na Borussia Monchengladbach, wakati RB Leipzig itacheza mechi matata kabisa na Borussia Dortmund.
Kwenye Serie A, Monza itacheza na Parma, huku Udinese ikimaliza ubishi na Hellas Veron, wakati AC Milan itakuwa San Siro kukabiliana na vijana wa Cesc Fabregas, Como 1907 na Torino itacheza na Empoli.
Kutakuwa na mechi tatu tu kwenye Ligue 1 kwa Jumamosi, ambapo Nantes itakuwa nyumbani kucheza na Lille, huku Angers ikiikaribisha AS Monaco na Lens itaulizana maswali magumu na Rennes.
Hivyo ndivyo hali ilivyo kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu tano bora huko Ulaya kwa wikiendi hii, ambapo Arsenal itajaribu kupunguza pengo la pointi dhidi ya Liverpool, ambayo wikiendi hii itakuwa kwenye majukumu mengine ya kuchuana na Newcastle United kwenye fainali ya Kombe la Ligi itakayopigwa uwanjani Wembley, Jumapili.
Kwenye La Liga pia moto utawaka, ambapo Barcelona, Real Madrid na Atletico ambazo ni timu tatu za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo, zitakuwa na mechi muhimu wikiendi hii kufahamu hatima yao kwenye mbio za ubingwa. Pointi moja tu inatofautisha miamba hiyo, ambapo endapo kama Madrid itashinda dhidi ya Villarreal itapanda kileleni na kuweka pengo la pointi, ambazo zinaweza kufikiwa na Barcelona ikitokea imepata matokeo ya ushindi ugenini mbele ya Atletico, ambako pia wataomba sare kwenye mechi ya Madrid huku wao wakipambana kuichapa Barcelona ili kushika usukani wa ligi hiyo. Moto utawaka.
Kwa mechi nyingine za Jumapili, Ligi Kuu England itashuhudiwa Fulham ikikipiga na Tottenham katika kipute cha London derby, huku Leicester City itakiwa King Power kucheza na Manchester United. Kwenye La Liga, Sevilla itacheza na Athletic Bilbao, Osasuna na Getafe na Real Vallecano itakipiga na Real Sociedad, wakati kwenye Bundesliga, burudani itakuwa baina ya VfL Bochum na Eintracht Frankfurt, FC Heidenheim itakipiga na Holstein Kiel na VfB Stuttgart itamaliza ubishi na vijana wa Xabi Alonso, Bayer Leverkusen.