Ujivuni wa Aurelio na kiburi cha Osimhen vilipokutana
Muktasari:
- Kuna wakati ilielezwa kwamba alifikia makubaliano binafsi ya kujiunga na Manchester City, lakini mwisho wa yote aliendelea kubaki Napoli.
KUANZIA 2019 hadi 2021 kilikuwa ni kipindi cha Kalodou Koulibaly kutajwa katika vyombo vya habari. Haikuwa inapita siku bila kusikia jina lake maeneo mbalimbali akihusishwa na timu kibao barani Ulaya.
Kuna wakati ilielezwa kwamba alifikia makubaliano binafsi ya kujiunga na Manchester City, lakini mwisho wa yote aliendelea kubaki Napoli.
Timu nyingi kubwa Ulaya ziliitaka huduma yake kwa sababu alikuwa mmoja kati ya mabeki bora zaidi barani humo muda huo, lakini ziligonga mwamba kabla ya Chelsea kufanikiwa kumnunua 2022 akiwa tayari ameshatimiza miaka 30.
Katika historia ya Napoli, mwaka 2004 timu hiyo ilifilisika na kushushwa daraja hadi Ligi Daraja la Tatu, lakini mwanaume mmoja, Aurelio De Laurentiis ambaye wakati huo kazi yake kubwa ilikuwa ni kutengeneza filamu aliinunua na kuweka mpango mkakati wa kuirudisha tena kwenye Ligi Kuu Italia (Serie A) na hilo lilifanikiwa ndani ya miaka mitatu. Aurelio ndiye Napoli na Napoli ni Aurelio. Baadhi ya viongozi na mawakala waliowahi kukaa na mzee huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 75, wanadai kuwa ni mmoja kati ya watu wagumu kufanya naye mazungumzo.
Katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi limetokea tukio lingine linalodhihirisha ugumu wa Aurelio linapokuja suala la usajili.
Inaelezwa kwamba Victor Osimhen alikuwa akitaka kuondoka tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, ambapo timu kibao zilionyesha nia ya kumsajili.
Lakini Aurielo alishikilia msimamo wa timu inayomtaka kutoa zaidi ya Pauni 100 milioni, jambo lililoshindikana.
Katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu, Osimhen alishachoshwa na hakuwa anataka tena kukaa Napoli, hivyo akawasilisha barua ya kuomba kuondoka. Napoli ilikubali, lakini kwa sharti la kupewa Pauni 111 milioni, pesa ambazo ilizirudisha nyuma timu nyingi.
Wakati Napoli inatakaa kiasi hicho, Osimhen naye alihitaji mshahara unaokaribia Pauni 500,000 kwa wiki.
Ilionekana wazi kwamba hakuna timu iliyokuwa tayari kutoa kiasi hicho cha pesa ukizingatia sheria za matumizi ya pesa zilizowekwa na Uefa zikionekana kuwabana sana katika kipindi hiki.
Siku zilivyoyoyoma, hatimaye bei ya Osimhen ikashushwa na Napoli ikasema inahitaji Euro 85 milioni.
Chelsea ilikuwa tayari kutoa pesa hiyo wakati Al Ahli ikiwa na Euro 80 milioni pekee. Aurelio na jopo lake ikachagua kwenda na ofa ya Chelsea.
Jambo baya ni kwamba mbali ya Chelsea kuwa tayari kutoa pesa hiyo, ilikuwa inataka kutoa mshahara wa Euro 4 milioni kwa mwaka wakati Ahli ikiwa tayari kutoa Euro 40 milioni.
Osimhen akakubali ofa ya Ahli, Aurelio na jopo lake wakakubali ofa ya Chelsea, mvutano huo uliendelea hadi dakika ya mwisho ya dirisha la usajili la England na Italia, hivyo Chelsea ikaikosa saini ya Mnigeria huyo.
Aurielo hakuwahi kuwa mtu wa kukubali kushindwa, kwani alifanya hivyo kwa Koulibaly katika madirisha kadhaa ya usajili, lakini raundi hii amekutana na kiburi cha Osimhen.
Licha ya Osimhen kuambiwa kwamba hatacheza ikiwa atakataa ofa ya Chelsea hakujadili na alikubali dirisha lifungwe.
Katika dirisha kama hili imewahi kutokea stori inayofanana na hii ambapo beki wa Manchester United, Leny Yoro aliambiwa na viongozi wa Lille kwamba akikataa kujiunga na mashetani hao wekundu watamweka nje na hatocheza msimu mzima kwa sababu waliweka pesa nyingi tofauti na ile ya Real Madrid, Yoro akakubali yaishe, lakini kauli hiyo haikufanya kazi kwa Osimhen.
Kwa sasa Aurelio amebakia na ujivuni wake wakati Osimhen amebaki na kiburi chake ingawa kwa Osimhen ambaye ameshajiunga na Galatasaray kwa mkopo alikubali kupoteza muda kwa kutokucheza wakati Aurelio akipoteza pesa kwani ilibidi staa huyo alipwe mshahara wake unaofikia Euro 9 milioni kwa mwaka.
Binafsi sikuwa naamini kama mambo yataendelea kuwa hivi hadi mwisho, ingawa dili la kwenda Saudi Arabia lilikufa kwani Ahli baada ya kuona mambo hayaeleweki iliamua kutua kwa Ivan Toney.
Wataalamu wa mambo walieleza kwamba ilikuwa ni ngumu kwa timu yoyote kumsajili Osimhen kwa mkataba wa kudumu kutokana na bei yake hivyo namna pekee ilikuwa ni kumchukua kwa mkopo kama ilivyofanya Galatasaray ambayo itaenda kumlipa mshahara wote wa msimu mzima.
Ikiwa Osimhen angeendelea kusalia ni Aurelio ndio alikuwa akionekana kupoteza zaidi kwani staa huyu angeendelea kuchukua mshahara hewa na kama angerudishwa katika timu itakuwa ni kushindwa kwa Aurelio, hivyo namna pekee ilikuwa ni kumtoa kwa mkopo ama kumuuza kwa pesa kiduchu na hatimaye wakakubali kumwachia kwa mkopo.