Ujauzito ulisababisha Oscar kumuua Reeva

Oscar Pistorius akiwa mahakamani kusikiliza kesi yake ya mauaji ya Reeva Steenkamp (picha ndogo) hivi karibuni nchini Afrika Kusini. Picha na AFP.
JOHANNESBURG, Afrika Kusini KIFO cha mwanamitindo Reeva Steenkamp kilichotokana na kupigwa risasi na rafiki yake wa kiume, mkimbiaji mlemavu wa miguu, Oscar Pistorius wa Afrika Kusini, kimezua taarifa zingine mpya. Inadaiwa kuwa, Pistorius alimuua kwa makusudi Steenkamp baada ya kubaini kuwa alikuwa na ujamzito wake. Kabla ya kumuua, alimsogeza kwenye kona ya eneo alilompiga risasi na kufanikisha dhamira yake ya mauaji, taarifa za ndani zilidai juzi nchini Afrika Kusini. Kama taarifa hizo zitakuwa na ukweli, ni wazi zitaongeza msuguano wa kesi hiyo tangu siku ile ya Valentine, ambapo Pistorius alimpiga risasi na kumuua mpenzi wake Steenkamp. Kwa sasa mkimbiaji huyo tajiri nchini Afrika Kusini yuko nje kwa dhamana. Katika madai yake, Pistorius anasema alimuua kwa bahati mbaya mpenzi wake akidhani au akimfananisha na mwizi aliyeingia ndani ya nyumba yake kupitia chumba cha bafu. Waendesha mashtaka katika kesi hiyo iliyovuta hisia nyingi, siyo tu nchini Afrika Kusini bali duniani kote, wanasema kuwa Pistorius alimpiga risasi na kumuua kwa makusudi mpenzi wake kufuatia kuzuka mzozo kati yao. Habari za ndani kufuatia uchunguzi huo, zinaonyesha kuwa polisi wanaamini mjamzito Steenkamp aliuawa baada ya kutoa taarifa za ujauzito wake. Mwili wake ulikutwa na majeraha manne ya risasi, kichwani, mkononi kifuani na sehemu ya kiuno. Katika kukumbuka kifo cha mpenzi wake, Pistorius alifanya ibada binafsi nyumbani kwa mjomba wake. Kabla ya kifo, majirani wa wapenzi hao wanasema walisikia mzozo kutoka kwenye nyumba ya Pistorius kabla ya polisi kuitwa, ambapo waliwatuliza na kuwataka kuacha kusumbua majirani. Saa chache kabla Steenkamp kupigwa risasi alionekana kupitia kamera za usalama barabarani akiwa kwenye gari karibu na nyumbani kwake.