Ujanja penalti za England siri ni hii

Muktasari:

  • Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida England ilifanya vizuri dhidi ya Uswisi katika robo fainali ya Euro na baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 katika dakika 120 ilienda kutinga nusu fainali kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

MUNICH, UJERUMANI: BAADA ya kumbukumbu mbaya ya kupoteza taji kwenye ardhi ya nyumbani mbele ya Italia kwa changamoto ya mikwaju ya penalti, kila shabiki alikuwa anahofia uwezo wa upigaji wa penalti wa wachezaji wa timu ya taifa ya England katika michuano ya Euro mwaka huu.

Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida England ilifanya vizuri dhidi ya Uswisi katika robo fainali ya Euro na baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 katika dakika 120 ilienda kutinga nusu fainali kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Mastaa wa Englan ikiwa pamoja na Cole Palmer, Jude Bellingham, Bukayo Saka, Ivan Toney na Trent Alexander-Arnold  ndio walipiga na kufunga zote, vilevile kipa  Jordan Pickford naye aliokoa penalti ya Manuel Akanji.

Taarifa zinadai moja ya siri za England kufanya vizuri kwenye upigaji wa penalti ni mafunzo waliyopewa na mtaalam wa masuala ya pumzi Stuart Sandeman ambaye pia ni mfanyakazi wa BBC Radio 1 anakohudumu kama DJ.

Stuart (41), aliwasili  kwenye kambi ya mazoezi ya England nchini Ujerumani wiki iliyopita na kupewa muda wa kuwafundisha wachezaji jinsi ya kupumua ili kusaidia utulivu wa neva, kushusha presha na kuongeza umakini.

Moja ya mafunzo aliyowapa ilikuwa ni kuvuta hewa ndani ya sekunde tano kisha kuitoa kwa sekunde hizo hizo pale wanapokuwa wanataka kufanya kitu na presha zao ziko juu.

Mwenyewe alieleza  mbinu hiyo inasaidia “kuruhusu misuli, tishu, mishipa na akili kuwa sawa, ili mchezaji afanye vizuri zaidi.”

Alisema kwa kiasi kikubwa alichokifundisha kinafanyiwa kazi ndio maana wachezaji wamekuwa wakifanya vizuri.

Wachezaji kama Palmer na Toney walionekana wakivuta pumzi ndani kabla ya kupiga penalti zao katika mchezo huo dhidi ya Uswisi na wakapata.

Kwa mujibu wa Luke Shaw, baada ya dakika 120 za mchezo wao dhidi ya Uswisi kumalizika,  Rice aliwakumbusha wachezaji wenzake wasisahau mbinu za kupumua wanapokwenda kupiga penalti.