UEFA yafanya mabadiliko mengine Ligi ya Mabingwa

Muktasari:
- Msimu wa 2024/25 ulishuhudia mfumo mpya wa kushirikisha timu 36 kwenye michuano hiyo, ambapo zilicheza kwa mtindo wa ligi. Na timu zilizomaliza nafasi nane za juu ziliingia moja kwa moja kama vinara kwenye hatua ya 16 bora.
ZURICH, USWISI: SHIRIKISHO la soka la Ulaya (UEFA) limepanga kufanya mabadiliko mengine kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu walipoanzisha mfumo mpya wa michuano hiyo.
Msimu wa 2024/25 ulishuhudia mfumo mpya wa kushirikisha timu 36 kwenye michuano hiyo, ambapo zilicheza kwa mtindo wa ligi. Na timu zilizomaliza nafasi nane za juu ziliingia moja kwa moja kama vinara kwenye hatua ya 16 bora.
Na timu 16 nyingine ziligomea nafasi nane kwa kucheza mtoano, nyumbani na ugenini na zile zilizopoteza hakukuwa tena na utaratibu wa zamani wa kuhamia kwenye Europa League.
Timu zilizoshika nafasi kuanzia 25 hadi 36 zilitupwa moja kwa moja nje ya michuano. Na sasa mashabiki wakiwa bado wanajaribu kuzoea mtindo mpya, Uefa inapanga kufanya mabadiliko mengine.
Na kinachoelezwa ni kwamba timu iliyomaliza nafasi ya juu kwenye mtindo wa ligi, itapewa faida ya kucheza mechi ya marudiano katika hatua ya 16 uwanja wa nyumbani. Na kwamba timu iliyomaliza nafasi ya kwanza na pili wakati wa mtindo wa ligi, itapewa nafasi ya kucheza nyumbani mechi ya marudiano kwenye hatua ya nusu fainali, endapo kama itafanikiwa kufikia raundi hiyo.
Na faida hiyo ya kucheza nyumbani mechi ya marudiano itahama kwa timu ambayo ilikuwa chini, lakini ilifanikiwa kuifunga timu ya juu iliyokuwa na hadhi hiyo.
Kwa mfano, timu iliyotinga hatua ya 16 kwa kupitia mechi za mchujo, ikiitoa timu iliyoongoza kwenye kipindi cha ligi, basi hadhi hiyo itahamia kwao, hivyo kwenye robo fainali, itacheza mechi ya marudiano kwenye uwanja wa nyumbani. Uefa inaamini, mabadiliko hayo yamepangwa ili kuchochea ushindani wa michuano hiyo kwenye hatua ya ligi ili kila timu kujaribu kumaliza juu kupata fursa nzuri mbele.