Trump kuibukia fainali ya Kombe la Dunia la Klabu
Muktasari:
- Habari hizo zimekuja siku moja baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kutangaza kuwa limefungua ofisi katika jengo la Trump Tower mjini New York.
NEW JERSEY, MAREKANI: Rais wa Marekani, Donald Trump amethibitisha kuwa atahudhuria fainali ya Kombe la Dunia la Klabu ya Fifa Jumapili huko New Jersey.
Habari hizo zimekuja siku moja baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kutangaza kuwa limefungua ofisi katika jengo la Trump Tower mjini New York.
Marekani imeandaa toleo la kwanza la Kombe la Dunia la Klabu iliyopanuliwa na itakuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka ujao, pamoja na Canada na Mexico.
Chelsea ilikuwa ya kwanza kukata tiketi ya kucheza fainali ya michuano hiyo iliyopangwa kufanyika Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa MetLife uliopo New Jersey, kufuatia kuifunga Fluminense mabao 2-0 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Julai 8, 2025. Mpinzani wa Chelsea amefahamika usiku wa jana Jumatano baada ya Paris St-Germain kucheza dhidi ya Real Madrid katika nusu fainali ya pili.
Trump, ambaye alihudhuria Super Bowl mwezi Februari mwaka huu, ni mwenyekiti wa kikosi kazi alichoanzisha kusimamia maandalizi ya kila mashindano.
Fifa tayari ina ofisi Miami na kuwepo Trump Tower kutaimarisha uhusiano wa shirika hilo na utawala wa Marekani.
“Tumepokea uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa serikali na rais na kikosi kazi cha White House kwa Kombe la Dunia la Klabu ya Fifa na Kombe la Dunia la Fifa mwaka ujao,” alisema Rais wa Fifa, Gianni Infantino.
“Fifa ni shirika la kimataifa na ili uwe wa kimataifa lazima uwe ndani, lazima uwe kila mahali, kwa hivyo lazima tuwe New York.”
Infantino amewahakikishia mashabiki kuwa watakaribishwa Marekani, licha ya kuwepo kwa taarifa za vizuizi vilivyowekwa na serikali ya nchi hiyo chini ya Trump kwa wahamiaji na marufuku ya kusafiri kwa nchi 12 ambapo inaelezwa marufuku hiyo inaweza kufika nchi 36.
Trump amekuwa na uwepo mkubwa zaidi katika michezo kwenye muhula wake wa pili, na kuwa rais wa kwanza aliyeketi kuhudhuria Super Bowl na kutangaza Mei kuwa Washington DC itakuwa mwenyeji wa Rasimu ya NFL ya 2027.
Trump pia amehudhuria hafla kadhaa za UFC, pamoja na onyesho la mwezi uliopita huko New Jersey, na amesema Ikulu ya White House itaandaa hafla ya UFC mwaka ujao.