Ueda aipeleka Japan hatua moja mbele, Tunisia yaaga Kombe la Dunia
Muktasari:
- Japan ilianza mechi hiyo kwa kasi na kufungua ukurasa wa mabao dakika ya nne kupitia Daichi Kamada aliyemalizia mpira uliotokana na shambulizi la haraka baada ya Tunisia kushindwa kuondoa hatari ndani ya eneo lao.
MONTERREY, MEXICO: JAPAN imeweka rekodi mpya kwenye Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Tunisia mabao 4-0 katika mchezo wa Kundi F uliochezwa kwenye Uwanja wa Estadio Monterrey, ushindi uliowafanya 'Samurai Blue' kukaribia kufuzu hatua ya 32 bora huku Tunisia ikigeuka taifa la tatu kuondolewa rasmi kwenye michuano hiyo.
Japan ilianza mechi hiyo kwa kasi na kufungua ukurasa wa mabao dakika ya nne kupitia Daichi Kamada aliyemalizia mpira uliotokana na shambulizi la haraka baada ya Tunisia kushindwa kuondoa hatari ndani ya eneo lao.
Baada ya bao hilo, Japan iliendelea kutawala mchezo kwa umiliki mkubwa wa mpira na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga huku kipa wa Tunisia, Aymen Dahmen, akifanya kazi kubwa.
Presha ya mshambulizi ya Japan hatimaye lilizaa matunda tena dakika ya 31 pale mshambuliaji Ayase Ueda alipofunga bao la pili kwa shuti kali, akionyesha ubora mkubwa wa safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Japan ikiwa mbele kwa mabao 2-0 huku Tunisia ikishindwa kabisa kutengeneza mashambulizi yenye madhara, jambo lililoonyesha tofauti kubwa ya kiwango kati ya timu hizo mbili.
Hata baada ya mapumziko, Japan iliendelea kuwa bora, Tunisia ilionekana kukosa mbinu na hamasa licha ya kocha mpya Hervé Renard kujaribu kuwahamasisha wachezaji wake.
Dakika ya 69, Japan iliongeza bao la tatu kupitia Junya Ito aliyemzidi nguvu beki wa Tunisia kabla ya kumalizia kwa utulivu.
Ueda alihitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao lake la pili katika mchezo huo kwa kichwa na hivyo kuwa mchezaji wa kwanza wa Japan kufunga mabao mawili katika mechi moja ya Kombe la Dunia.
Mbali na ushindi huo kuwa mkubwa kwa Japan, pia uliweka rekodi kwani ni mara ya kwanza kwa taifa hilo kufunga mabao manne katika mchezo mmoja wa Kombe la Dunia.
Kwa upande wa Tunisia, matokeo hayo yameongeza presha baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo minane kati ya tisa iliyopita, hali iliyowafanya waage rasmi mashindano hayo wakiwa hawajaonyesha kiwango kilichotarajiwa.
Ushindi huo umeifanya Japan kufikisha pointi nne katika Kundi F na sasa inahitaji angalau sare dhidi ya Sweden katika mchezo wake wa mwisho wa kundi ili kujihakikishia tiketi ya moja kwa moja kwenda hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026.