Mabao 100 mechi 33, kuna nini Amerika Kaskazini?
Muktasari:
- Rekodi mpya ni kufikisha mabao 100 ndani ya michezo 33 pekee, jambo ambalo halijawahi kutokea kwa kasi hiyo tangu mwaka 1958.
NEW YORK/ TORONTO: KOMBE la Dunia 2026 huko Amerika ya Kaskazini katika mataifa ya Mexico, Canada na Marekani linaendelea kutoa burudani huku likivunja rekodi moja baada ya nyingine.
Rekodi mpya ni kufikisha mabao 100 ndani ya michezo 33 pekee, jambo ambalo halijawahi kutokea kwa kasi hiyo tangu mwaka 1958.
Bao la 100 lilifungwa na mshambuliaji wa Uholanzi, Cody Gakpo, katika ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Sweden, matokeo yaliyoendelea kuthibitisha kuwa michuano ya mwaka huu imejaa mabao.
Kwa mujibu wa takwimu, ni Kombe la Dunia la mwaka 1954 pekee nchini Usiwisi lililofikia mabao 100 kwa kasi zaidi, likihitaji michezo 20 tu. Baada ya hapo, mashindano mengi yalihitaji muda mrefu zaidi kufikia idadi hiyo.
Kombe la Dunia la Brazil mwaka 2014 lilihitaji michezo 36 kufikisha mabao 100, sawa na mwaka 1982 huku yale ya Argentina 1978 na Marekani 1994 yakihitaji michezo 38.
Kwa wastani wa mabao 3.09 kwa kila mchezo, Kombe la Dunia 2026 linaelekea kuvunja rekodi nyingi zaidi na huenda likafikisha zaidi ya mabao 300 kabla ya bingwa mpya kutangazwa.
MPIRA WA TRIONDA UNAWASUMBUA?
Swali kubwa ambalo wengi wanauliza ni kwanini mabao yanaongezeka kwa kasi kiasi hiki?
Jibu la kwanza linaweza kuwa mpira mpya wa Adidas Trionda unaotumika katika michuano hiyo.
Tayari kumekuwa na dalili kwamba walinda mlango wengi wanapata shida kusoma mwelekeo wa mpira huo hasa kwenye mashuti ya mbali. Mpira huo unaonekana kubadilika kasi na mwelekeo ghafla hali inayowapa ugumu makipa.
Mfano mkubwa ulionekana wakati Kylian Mbappe alipoifungia Ufaransa bao la pili dhidi ya Senegal kwa shuti la umbali wa zaidi ya mita 27 lililomshinda kipa Edouard Mendy.
Katika raundi ya kwanza pekee, mabao matano yalifungwa kutoka umbali wa zaidi ya mita 20. Yasin Ayari wa Sweden alifunga mawili dhidi ya Tunisia, huku Connor Metcalfe wa Australia na Ismael Saibari wa Morocco wakiongeza orodha ya mabao ya mbali yaliyowashangaza makipa.
Kipa wa zamani wa England, Joe Hart, amekiri kuona makipa wakipata shida kuudhibiti mpira huo mpya.
"Huu ni mpira ambao wakati mwingine unafanya mambo ambayo hujayatarajia," anasema Paul Robinson, kipa mwingine wa zamani wa England.
Hali hii inawakumbusha wengi Kombe la Dunia la mwaka 2010 nchini Afrika Kusini ambapo mpira wa Jabulani uliibua malalamiko makubwa kutokana na tabia yake ya kubadilika angani na kuwatesa makipa.
TIMU 48 ZIMECHANGIA?
Kombe hili ni la kwanza kushirikisha timu 48 tofauti na 32 zilizokuwepo awali.
Kuongezeka kwa timu kumetoa nafasi kwa mataifa mapya kama Cape Verde, Curacao, Jordan na Uzbekistan kushiriki kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Ingawa baadhi ya timu hizo zimeonyesha ushindani mkubwa, bado kuna mechi ambazo zimeonyesha tofauti ya viwango.
Curacao ilijikuta ikipokea kipigo cha mabao 7-1 kutoka Ujerumani huku Canada ikiichapa Qatar mabao 6-0.
Hata hivyo, si kila mtu anakubaliana kwamba timu ndogo ndizo chanzo kikuu cha mabao mengi.
Kocha Thomas Frank anaamini tofauti ya viwango imeonekana katika mechi chache tu na kwamba timu nyingi zimeonyesha uimara mkubwa kuliko ilivyotarajiwa.
Mfano mzuri ni Cape Verde ambao waliinyoosha Hispania kwa sare ya bila kufungana katika moja ya matokeo yaliyoshangaza zaidi katika hatua ya makundi.
MAPUMZIKO MAREFU KATI YA MECHI
Tofauti na mashindano mengi yaliyopita, ratiba ya mwaka huu imezipa timu muda mkubwa zaidi wa kujiandaa kati ya mchezo mmoja na mwingine.
Mexico ilicheza mechi ya ufunguzi Juni 11 lakini ikasubiri karibu wiki moja kabla ya kucheza mchezo wake uliofuata.
Muda huo wa ziada umewasaidia nyota wengi kurejesha nguvu, kupona majeraha madogo na kuingia uwanjani wakiwa katika kiwango bora.
Athari yake inaonekana moja kwa moja kwenye idadi ya mabao.
JOTO LINACHANGIA KUCHOKA MABEKI
Mashindano haya yanafanyika katika kipindi cha kiangazi cha Amerika Kaskazini ambapo baadhi ya miji imekuwa na joto kali.
Takwimu zinaonyesha mabao 30 kati ya 105 yaliyofungwa hadi sasa yamepatikana kuanzia dakika ya 76 hadi mwisho wa mchezo.
Hiyo ni karibu asilimia 29 ya mabao yote.
Takwimu hizo zinaonyesha wazi kwamba kadri mechi zinavyoelekea mwisho, wachezaji wengi wanapoteza nguvu na kufanya makosa ambayo yanawapa wapinzani nafasi za kufunga.
Tunisia ni mfano mzuri baada ya kufanya makosa kadhaa dhidi ya Sweden yaliyozaa mabao manne katika kipigo cha mabao 5-1.
MAPUMZIKO YA MAJI YAMEBADILI MBINU
Mbali na kuwapa wachezaji nafasi ya kunywa maji, mapumziko ya lazima ya dakika tatu yamekuwa silaha mpya kwa makocha.
Katika muda huo mfupi, makocha wanapata nafasi ya kurekebisha mfumo, kutoa maelekezo mapya na hata kuwaonyesha wachezaji video za makosa waliyoifanya.
Morocco iliongoza dhidi ya Brazil kabla ya mapumziko ya maji, lakini muda mfupi baada ya mchezo kurejea, Brazil walifanikiwa kusawazisha.
Kocha wa Uswisi, Murat Yakin, amesema mapumziko hayo yamekuwa kama muda mfupi wa ziada wa kufanya mazungumzo ya kiufundi.
"Ndani ya dakika tatu tunaweza kuzungumza kuhusu mabadiliko, mbinu na hata kuwaonyesha wachezaji picha za makosa yao," anasema Yakin.
NYOTA WAKUBWA WAMEWASILI KAMILI
Sababu nyingine kubwa ya mabao mengi ni kwamba mastaa wakubwa wameanza mashindano katika kiwango bora.
Lionel Messi tayari amefunga hat-trick dhidi ya Algeria na kusawazisha rekodi ya mabao ya Kombe la Dunia iliyokuwa ikishikiliwa na Miroslav Klose.
Mbappe ameanza kwa mabao mawili dhidi ya Senegal, Vinicius Junior amefunga katika mechi zote mbili za Brazil, huku Erling Haaland na Harry Kane nao wakianza kwa kasi ya juu.
Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, nyota wengi wamewasili kwenye Kombe la Dunia wakiwa hawana majeraha makubwa wala uchovu wa msimu.
Hilo limeongeza ubora wa mashambulizi na kuifanya michuano kuwa na mabao mengi zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
REKODI ZAIDI ZINAKUJA?
Kwa wastani wa mabao zaidi ya matatu kwa kila mchezo na huku hatua za mtoano zikiwa bado hazijaanza, kila dalili zinaonyesha Kombe la Dunia 2026 linaweza kuwa miongoni mwa matoleo yenye mabao mengi zaidi katika historia.
Mpira mpya, joto kali, mfumo wa timu 48, mapumziko ya maji na ubora wa nyota waliopo vyote vinaonekana kuchangia.
Lakini jambo moja ambalo halina mjadala ni kwamba mashabiki duniani kote wanashuhudia moja ya Kombe la Dunia lenye burudani kubwa zaidi kuwahi kuchezwa.