Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ubingwa Ulaya ulivyopagawisha ndoa ya Carol wa Marquinhos

Muktasari:

  • PSG walichukua ubingwa huo ikiwa ni mara ya pili mfululizo baada ya kuifunga Arsenal kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika dimba la Puskás Aréna nchini Hungary.

BAADA ya Paris Saint-Germain (PSG) kutwaa tena taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, mafanikio hayo yamemuacha na mshangao na furaha kubwa mke wa mchezaji wa klabu hiyo, Marquinhos, Carol Cabrino, ambaye hajasita kueleza hisia zake.

PSG walichukua ubingwa huo ikiwa ni mara ya pili mfululizo baada ya kuifunga Arsenal kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika dimba la Puskás Aréna nchini Hungary.

"Mara mbili juu ya kilele cha michuano ya Ulaya. Umeandika jina lako katika historia, na ninashukuru kuwa ninaishi na kushuhudia yote haya nikiwa kando yako. Asante, PSG. Bado siamini kabisa kwamba haya yote yametokea!," aliandika Carol.

Je, Carol ni nani hasa? Carol alizaliwa Julai 29, 1993, katika jiji la São Paulo, Brazil. Alisoma sekondari katika The International School of São Paulo, na baada ya hapo alisomea Shahada ya Sanaa katika Lugha ya Kiingereza katika Chuo Kikuu cha São Paulo.

Mrembo huyu ametokea katika familia ambayo inajiweza kiuchumi, ambapo wazazi wake walimuunga mkono katika kipaji chake cha uimbaji kwani tangu akiwa mdogo alipenda muziki, na alifanya kazi kwa bidii ili kutimiza ndoto yake ya kuwa mwimbaji maarufu.

Safari yake ya muziki ilianza kung’ara baada ya kushiriki katika kipindi cha kusaka vipaji vya uimbaji nchini Brazil kinachoitwa Jovens Talentos, ambacho hufananishwa na X Factor. Carol alipata umaarufu mkubwa alipofanya cover ya wimbo wa Katy Perry, Roar (2013).

Kwa sasa, akitambulika na wengi kama mshawishi wa chapa maarufu kutoka Brazil, bado Carol ameendelea na kazi yake ambapo ana chaneli yake ya YouTube ambayo huweka nyimbo zake za muziki wa asili.

Amewekeza katika kazi zake kama mwimbaji na mtayarishaji wa maudhui mtandaoni. Hata hivyo, kwa wakati huu amejikita zaidi katika mitandao ya kijamii kama Instagram na YouTube, ambako anazidi kupata umaarufu kupitia maudhui anayoposti.

Umaarufu wake katika burudani na mitandao ya kijamii umeongeza zaidi hamu kwa mashabiki kufuatilia maisha yake binafsi, shughuli zake mbalimbali na mafanikio ya mume wake katika ulimwengu wa soka.

Mnamo Mei 2015, Marquinhos aliliambia gazeti la Le Parisien kwamba alikuwa amemvisha pete ya uchumba mwimbaji huyo, tukio lililofanyika katika Mnara wa Eiffel nchini Ufaransa.

Wawili hao walifunga ndoa Juni 2016, na kufikia Mei 2017 walitangaza kuwa wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza.

Carol alikuwa na furaha kubwa hadi kuingia mtandaoni na kuandika ujumbe mrefu, pamoja na kuposti video ya mumewe akitokwa na machozi ya furaha baada ya kupata habari hiyo.

"Tumefanya kila kitu kwa namna tuliyotamani, sivyo? Tulikutana, tukapendana, tukafunga ndoa… na sasa tuko katika hatua yetu nzuri zaidi, ujauzito! (Na katika mwezi tulioutamani!).

"Mungu amefanya kila kitu kwa ukamilifu kiasi kwamba leo ninachoweza kufanya ni kumshukuru kwa kukuleta katika maisha yangu. Kwa kunipa zawadi na heshima ya kujifunza mambo mengi kupitia wewe na nikiwa kando yako," alieleza Carol.

Mtoto wao wa kwanza alizaliwa Novemba 1, 2017. Inaelezwa kuwa Carol alishikwa na uchungu wakati akimtazama Marquinhos akicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya R.S.C. Anderlecht katika Uwanja wa Parc des Princes.

Kwa ujumla, hadi sasa wawili hao wana watoto wanne ambao ni Maria (2017), Enrico (2019), Marina (2022) na Filippo (2026). Familia hiyo inaishi nchini Ufaransa kwa sababu Marquinhos bado ana kibarua cha kuichezea PSG.

Machi 2025, Carol aliposti video kwenye Instagram ambapo alielezea kwa masikitiko makubwa tukio la kupoteza ujauzito wake wa wiki tisa.

"Nitazungumza kuhusu jambo ambalo si zuri sana. Lakini nimekubali kilichonitokea na ninataka kuwashirikisha kwa sababu najua wengi wenu mmepitia hali kama hii," alisema.

Kwa mujibu wa maelezo yake, kila kitu kilikuwa kinaenda sawa, lakini alipoenda hospitali kufanyiwa kipimo cha ultrasound, madaktari walimueleza kuwa mapigo ya moyo ya mtoto yamesimama na hakuna dalili zozote za uhai wa mtoto huyo.

Alieleza kuwa hali hiyo ilikuwa ngumu zaidi kwa sababu mume wake, Marquinhos, alikuwa mbali akiwa na timu ya taifa ya Brazil wakati tukio hilo lilipotokea. Baada ya kupitia kipindi hicho kigumu, Carol alisema anaelekeza nguvu zake katika kuwatunza watoto wake pamoja na familia yake.