Tunisia yajipa matumaini Afcon 2025
Muktasari:
- Miamba hiyo inafahamu huzuni inayowakabili baada ya kufanya hovyo kwenye Afcon 2023 na ilikomea hatua ya makundi katika mashindano hayo, haikushinda mechi yoyote kati ya tatu ilizocheza.
RABAT, MOROCCO: TUNISIA inaamini itaanza vizuri kabisa katika kampeni yao ya kusaka ubingwa wa Afrika wakati wa mashindano ya Afcon 2025 ambapo mechi ya kwanza itakipiga na Uganda kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Rabat, Jumanne.
Miamba hiyo inafahamu huzuni inayowakabili baada ya kufanya hovyo kwenye Afcon 2023 na ilikomea hatua ya makundi katika mashindano hayo, haikushinda mechi yoyote kati ya tatu ilizocheza.
Sasa kikosi hicho kinachonolewa na Sami Trabelsi kitakwenda Morocco baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye mechi za kufuzu nyuma ya Comoros baada ya kushinda mechi tatu, sare moja na vichapo vizuri.
Tunisia ilijiandaa kwa mechi za Afcon 2025 kwa kucheza kipute cha kirafiki dhidi ya Botswana na kushinda 2-1 na ilicheza kwenye mashindano ya Arab Cup mapema mwezi huu, lakini haikufanya vizuri zaidi ya hatua ya makundi.
Tunisia ilipoteza kwa 1-0 dhidi ya Syria, ilitoka sare ya 2-2 dhidi ya Palestine na kuichapa Qatar 3-0, na matokeo hayo yaliwafanya kumaliza nafasi ya tatu kwenye kundi na hivyo kushindwa kutinga hatua ya robo fainali.
Uganda inarejea kwenye mashindano ya Afcon kwa mara ya kwanza tangu 2019 baada ya kushindwa kufuzu awali mbili zilizopita. Kikosi hicho cha Kocha Paul Put kilichuana na Afrika Kusini na kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi K na ilizidiwa na timu iliyoshika namba moja kwa tofauti ya pointi moja tu.
Uganda ilipoteza mechi moja kati ya sita ilizocheza kwenye kundi lao, ilipochapwa 2-0 na Bafana Bafana, Novemba 15, 2024 baada ya kutoka nao sare ya 2-2 katika mechi ya kwanza, huku ilishinda mechi nne zilizobaki.