Victor Osimhen atuma ujumbe kwa mashabiki
Muktasari:
- Kikosi hicho cha Super Eagles kimewasili huko Morocco kwenye mashindano ya Afcon 2025 kikiwa na mzigo mzito wa kuhakikisha kinafikia malengo makubwa ili kuondoa uchungu kwa mashabiki wao.
RABAT, MOROCCO: STRAIKA wa Nigeria, Victor Osimhen amesema Afcon 2025 ni sehemu mwakafa ya kuponyesha vidonda vyao na kuwapa mashabiki kile wanachostahili baada ya kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
Kikosi hicho cha Super Eagles kimewasili huko Morocco kwenye mashindano ya Afcon 2025 kikiwa na mzigo mzito wa kuhakikisha kinafikia malengo makubwa ili kuondoa uchungu kwa mashabiki wao.
Mabingwa hao mara tatu wa Afrika wameshindwa kukamatia tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico baada ya kufungwa na DR Congo kwenye mechi ya mchujo iliyofanyika Morocco mwezi uliopita.
Nigeria sasa imejipanga upya ikirudi Morocco kwa ajili ya mashindano tofauti kabisa na itarusha kete yake ya kwanza kwenye Afcon, kesho Jumanne itakapomenyana na Tanzania uwanjani Fez, ikiwa imepangwa Kundi C sambamba na timu za Tunisia na Uganda.
Imani kwa mashabiki imeshuka kutokana na timu hiyo kushindwa kufanya vizuri katika mashindano makubwa, huku takwimu zikiitaja Nigeria na mataifa mengine kama Morocco, Misri, Algeria na Senegal kuwa nchi zinazopewa nafasi kubwa ya kushinda ubingwa wa Afcon 2025.
Akizungumza baada ya kufanya mazoezi uwanjani Fez, Jumapili, straika huyo wa Super Eagles amesema anatambua mashabiki wamekataa tamaa na kwamba wana vidonda kwenye mioyo yao ambavyo vinapaswa kutibiwa.
“Tunafahamu huzuni yao. Tulijitolea kila kitu kufuzu Kombe la Dunia, lakini penalti wakati mwingine ni kitu cha bahati, wakati mwingine unashinda na kipindi kingine unafungwa,” amesema Osimhen.
“Sasa tuna nafasi hii ya kurudisha mioyo ya mashabiki wetu. Nataka kuwashukuru mashabiki wa Super Eagles ambao huwa wamekuwa hawakati tamaa tukipita kwenye mapito yote mazuri na mabaya. Afcon hii ni wakati wa kuandika historia mpya.”
Licha ya kuwa straika hatari kwa mabao, akiifungia Nigeria mara 31 katika mechi 46, Osimhen amekuwa na wakati mgumu kwenye Afcon na amefunga mara moja katika mechi nane alizocheza katika Afcon 2019 na Afcon 2023.
“Tunakwenda vitani, ” amesema Osimhen akijaribu kutuma ujumbe kwa wapinzani wao katika Kundi C na timu nyingine zitakazokutana na Nigeria katika mikikimikiki hiyo ya Afcon 2025.
Super Eagles inataka kurudia mafanikio ya Afcon 2023, ambapo ilifika fainali na kuchapwa 2–1 na Ivory Coast.