Tunachukue

Tuesday April 20 2021
man pic

MANCHESTER, ENGLAND. INAWEZA kuwa moja kati ya matukio ya kushangaza katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni ikiwa Manchester United itafanikiwa kuipiku Manchester City na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu kutokana na idadi ya pointi ambazo imepitwa.

Lakini kwa mujibu wa kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer mambo ya kushangaza kwenye soka huwa yanatokea hivyo kwake kuipiku Man City na kuchukua ubingwa kwa msimu huu ni jambo linalowezekana.

Man United jana ilikuwa na kibarua dhidi ya Burnley na ilikuwa ni fursa ya kwanza ya kupunguza pengo la pointi kati yake na Man City na timu zote zimebakisha mechi sita.

Ushahidi unaonyesha kuwa timu iliyowahi kuangusha ubingwa wakati ilishakuwa mbele kwa tofauti ya alama nane ni Man United yenyewe kwenye msimu wa 1997-98 na 2011-12 mbele ya Arsenal na Man City ambayo ilifanya maajabu hayo chini ya Roberto Mancini baada ya Sergio Aguero kufunga bao lile la kihistoria la ‘Aguerooooo!” katika dakika za mwisho kwenye mchezo dhidi ya QPR na kusababisha Man City iongoze msimamo wa tofauti ya mabao.

Ushindi ambao Man United iliupata msimu huu dhidi ya Man City na kipigo ambacho timu hiyo ilipokea kutoka kwa Leeds United imekuwa moja kati ya mambo yanayoashiria kwamba huenda upepo ukabadilika na maajabu yakageukia kwa Man United.

“Kila mechi ni muhimu kwa Manchester United na hatutakubali kuachia pointi kizembe kwenye mechi zetu zijazo, unaniuliza kama tunaweza kuipata Man City? Mambo ya ajabu huwa yanatokea kwenye soka, yule anayeongoza anaweza kuanguka, ni kweli wana kikosi imara na wana matumaini makubwa ya kupata taji, “Ninachokiamini ni kufanya kazi yetu kwa ufasaha ikiwa pamoja na kushinda kila mechi ya ligi iliyo mbele yetu na baada ya hapo ndio tutawaangalia wao kama watapoteza au la,” alisema Solskjaer na kuongeza:

Advertisement

“Hatuwezi kukibadili kile wanachofanya, tunatakiwa kucheza mechi zetu na ukizingatia tuna mechi ngumu nyingi mbele yetu.”

Man United imekuwa na kiwango bora tangu ipoteze kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Leicester City ikiwa imeshinda mechi mbili za Ligi Kuu na zile za Europa League dhidi ya Granada kuanzia ile ya nyumbani na ugenini.

Miongoni mwa wachezaji wanaonekana kuwa moto kwenye kikosi hicho katika michezo hiyo minne ni Mason Greenwood ambaye amefunga mabao matatu katika mechi zake tano za mwisho baada ya mechi 26 zilizotangulia kufunga bao moja tu.

“Mason amekuwa bora sana msimu huu, unaweza kuangalia hata mwili wake umejengeka na amekuwa imara sasa, vilevile amekuwa na muendelezo wa kucheza kwa kiwango cha juu na nina imani ataanza kufunga mabao mengi kwenye siku zijazo, ninavutiwa naye sana na nina furaha ya kuona maendeleo yake kwa msimu huu,” aliongeza Solskjaer.

Man United pia ipo kwenye nafasi nzuri ya kuchukua taji la Europa League kwa msimu huu ambako imeingia kwenye hatua ya nusu fainali na itaumana na Roma.

“Kumaliza bila taji msimu uliopita ni miongoni mwa mambo yaliyotuumiza sana lakini muda mwingine kuanguka kutakufanya uendelee kuwa chini au kusimama tena, tumepoteza nusu fainali nne hadi sasa na nimeona jinsi wachezaji walivyo na ari ya kupambana ili kushinda hizi mechi zilizo mbele yetu.”

Advertisement