Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tudor apata ushindi wa kwanza Spurs ikitupwa nje UEFA

Muktasari:

  • Spurs walikuwa na kazi ngumu baada ya kufungwa 5-2 katika mechi ya kwanza huko Madrid, moja ya vipigo vinne ndani ya mechi tano tangu Tudor alipomrithi Thomas Frank kama kocha.

TOTTENHAM Hotspur wamepata ushindi wa kwanza chini ya kocha Igor Tudor dhidi ya Atletico Madrid lakini wameshindwa kufuta pengo la mabao matatu, hivyo wametolewa kwenye Ligi ya Mabingwa hatua ya 16 bora.

Spurs walikuwa na kazi ngumu baada ya kufungwa 5-2 katika mechi ya kwanza huko Madrid, moja ya vipigo vinne ndani ya mechi tano tangu Tudor alipomrithi Thomas Frank kama kocha.

Hata hivyo, kiwango chao kiliongezeka kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Liverpool katika mechi ya Premier wikiendi iliyopita, jambo linalowapa matumaini wanapogeukia lengo lao kuu la kuepuka kushuka daraja kwenye Ligi Kuu England.

Spurs walihitaji bao la kwanza na walianza vizuri, wakifunga dakika ya 30 kupitia kichwa cha Randal Kolo Muani baada ya kupokea krosi nzuri kutoka Mathys Tel, likiwa bao lake la nne kwenye mashindano msimu huu.

Tel alipata nafasi nyingine nzuri kuongeza bao lakini kipa wa Atletico, Juan Musso aliyechukua nafasi majeruhi Jan Oblak, alifanya uokozi muhimu.

Kwa upande mwingine, Guglielmo Vicario aliokoa mashambulizi ya Julian Alvarez na Giuliano Simeone.

Dakika mbili baada ya kipindi cha pili kuanza, Atletico walipunguza kwa bao la Alvarez aliyefunga shuti kali lililoingia kona ya juu.

Spurs walilalamika kuwa Xavi Simons alifanyiwa madhambi kabla ya bao hilo, ambapo Alvarez aliongoza shambulizi la kushtukiza na kumalizia pasi ya Ademola Lookman.

Hata hivyo, Simons alijibu haraka kwa kuifungia Spurs bao la pili kwa shuti la chini lililopinda dakika tano baadaye.

Vijana wa kocha Diego Simeone walikuwa chini ya presha kubwa, wakimshukuru Musso kwa kuokoa michomo ya Pedro Porro na Radu Dragusin.

Umuhimu wa uokozi huo ulionekana pale Atletico walipokatiza matumaini ya Spurs kwa bao la pili dakika 15 za mwisho, lililofungwa na David Hancko kwa kichwa baada ya kona ya Alvarez.

Atletico waliweza kupumua kwa afueni walipojihakikishia kufuzu na sasa watakutana na Barcelona katika robo fainali.

Bao la penalti la dakika za mwisho la Simons baada ya kuchezewa vibaya na Jose Maria Gimenez, liliwapa Spurs ushindi wa 3-2 usiku huo wa Machi 18, 2026, lakini wametupwa nje kwa jumla ya mabao 7-5.

Sasa Spurs wataelekeza nguvu zao kwenye mechi muhimu ya ligi dhidi ya Nottingham Forest Jumapili wiki hii, katika vita ya kuepuka kushuka daraja.