'Hydration break' yazua mjadala Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Katika fainali hizo ambazo zinafanyika Marekani, Canada na Mexico kuna utaratibu wa dakika tatu wa kunywa maji katika kila kipindi kwa lengo la kulinda afya za wachezaji kutokana na hali ya joto kali.
NEW YORK, MAREKANI: FAINALI za Kombe la Dunia 2026 zimeendelea kushika kasi Amerika Kaskazini, lakini muda mapumziko ya kunywa maji (hydration break) umezua mjadala.
Katika fainali hizo ambazo zinafanyika Marekani, Canada na Mexico kuna utaratibu wa dakika tatu wa kunywa maji katika kila kipindi kwa lengo la kulinda afya za wachezaji kutokana na hali ya joto kali.
Lakini, kadri mashindano yanavyoendelea, mjadala unaongezeka kuhusu kama mapumziko hayo yanalinda afya za wachezaji au yanabadilisha sura ya mchezo wa soka.
Kwa mara ya kwanza baadhi ya mashabiki wameanza kuhisi mchezo wa soka unageuka kutoka wa vipindi viwili kwenda vinne kama ilivyo kwenye michezo ya mpira wa kikapu na soka la Kimarekani (American Football).
Katika viwanja mbalimbali, mashabiki wameonekana wakipiga kelele za kupinga mapumziko hayo wakiamini yanaua kasi ya michezo na kuathiri msisimko wa mashindano.
Nahodha wa Uholanzi, Virgil van Dijk ni miongoni mwa waliokosoa mfumo huo, akisema mapumziko hayo yanavuruga mtiririko wa mchezo.
Kwa upande wake, nahodha wa Ufaransa, Kylian Mbappe alisema wakati mwingine mapumziko hayo yanaweza kusaidia, lakini yana uwezo wa kuvuruga kasi ya timu inayocheza vizuri.
Licha ya mjadala huo, takwimu zinaonyesha kuwa mapumziko hayo tayari yana athari kubwa ndani ya uwanja.
Katika mabao 140 yaliyofungwa katika raundi mbili za kwanza za hatua ya makundi, mabao 31 (sawa na asilimia 22.1) yalifungwa ndani ya dakika tano kabla au baada ya mapumziko ya kunywa maji.
Kinachovutia zaidi ni kwamba mabao 18 kati ya hayo yalibadilisha matokeo ya mchezo kwa kuipa timu uongozi au kuisawazishia mabao.
Wachambuzi wa soka wanaamini timu nyingi zimeanza kutumia dakika chache kabla ya mapumziko hayo kuongeza kasi ya mashambulizi zikijua muda wa kupumzika unakaribia.
Mbinu hiyo imeonekana kuzisaidia zaidi timu kubwa ambazo zina wachezaji wengi wenye uwezo wa kuongeza kasi ya mchezo kwa muda mfupi kabla ya kupata nafasi ya kupumzika.
Japan ni moja ya timu zilizofanikiwa kutumia vyema mazingira hayo baada ya kufunga bao dakika nne baada ya mapumziko ya kwanza dhidi ya Tunisia na kuongeza lingine dakika chache kabla ya mapumziko ya pili katika ushindi wao wa mabao 4-0.
Canada nayo imeonyesha uwezo wa kutumia nyakati hizo muhimu huku baadhi ya timu zikionekana kushindwa kabisa kurejea katika mdundo wao baada ya mchezo kusimamishwa.
Ingawa FIFA imeendelea kusisitiza kuwa afya na ustawi wa wachezaji ndio sababu kuu ya kuanzishwa kwa mfumo huo, baadhi ya wadau wanaamini mapumziko hayo yana manufaa ya kibiashara kutokana na uwepo wa wadhamini wanaotumia muda huo kujitangaza.
Hata hivyo, jambo moja ambalo haliwezi kupingwa ni kwamba mapumziko hayo tayari yamebadili namna mechi zinavyochezwa katika Kombe la Dunia mwaka huu.
Kwa sasa makocha, wachezaji na wachambuzi wanalazimika kupanga mikakati mipya wakijua kuwa ndani ya kila kipindi kuna muda ambao unaweza kubadili kabisa mwelekeo wa mchezo.
Wakati FIFA ikiendelea kutetea mfumo huo, tayari Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) limethibitisha kuwa hakutakuwa na mapumziko ya lazima ya kunywa maji katika Euro 2028 isipokuwa pale hali ya hewa itakapolazimisha.