Tuchel apewa ramani ya kumfunga Messi
Muktasari:
- Kikosi cha Lionel Scaloni kina silaha nyingi, kuanzia kwa nahodha wake Lionel Messi, ambaye akiwa na miaka 39 bado anaamua matokeo ya mechi makubwa. Hata hivyo, mechi dhidi ya Uswisi, kama zilivyokuwa zile za Cape Verde na Misri, zilionyesha wazi kuwa Argentina pia ina mapungufu.
ATLANTA, MAREKANI: ARGENTINA inaonekana inafungika. Tatizo ni kwamba hakuna anayefanikiwa kuifunga. Hilo ndilo fumbo ambalo kocha wa England, Thomas Tuchel, anatakiwa kulitatua kabla ya pambano la nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Kikosi cha Lionel Scaloni kina silaha nyingi, kuanzia kwa nahodha wake Lionel Messi, ambaye akiwa na miaka 39 bado anaamua matokeo ya mechi makubwa. Hata hivyo, mechi dhidi ya Uswisi, kama zilivyokuwa zile za Cape Verde na Misri, zilionyesha wazi kuwa Argentina pia ina mapungufu.
Kazi ya Tuchel ni kuyatumia mapungufu hayo ipasavyo ili kuhakikisha moyo wa kupambana wa Argentina na uamuzi yoyote yenye utata ya waamuzi hayazuii England kutinga fainali.
- Messi bado ndiye silaha kuu
Dhidi ya Uswisi, Messi hakuwa katika kiwango chake bora kama ilivyokuwa kwenye mechi zilizopita, lakini bado alionyesha ubora wake.
Ni yeye aliyepiga kona iliyomkuta Alexis Mac Allister, aliyefunga bao la kwanza. Pasi hiyo ilimfanya Messi kuweka rekodi mpya ya pasi za mabao nyingi zaidi katika historia ya Kombe la Dunia, sambamba na rekodi yake ya mabao.
Pia, alipata nafasi kadhaa za kufunga, ikiwemo shuti la mguu wa kulia lililopita kidogo pembeni mwa lango.
Messi hucheza kama mshambuliaji anayeshuka chini kutafuta mpira katika mfumo unaofanana na 4-4-2. Takwimu zinaonyesha hutembea kwa takribani asilimia 60 ya muda wa mchezo na kusimama kwa karibu asilimia 20 nyingine.
Lakini katika asilimia iliyobaki, anapokuwa na mpira miguuni, huwa vigumu sana kuzuilika.
England italazimika kukata njia zote za kumpatia pasi na kubana eneo la katikati, ambako Messi hupenda kucheza.
Uswisi ilifanya kazi hiyo vizuri kwa kubaki na safu iliyobana na kuziba njia za pasi kuelekea kwa Messi pamoja na Julian Alvarez.
Huenda usimzuie Messi kwa dakika zote 90, lakini unaweza kumzuia asiutawale mchezo na kupunguza nafasi zake za kuamua matokeo.
2. Si Messi pekee anayebeba hatari
Mbali na Messi, Argentina ina wachezaji wengine wenye uwezo mkubwa wa kubadilisha matokeo.
Dhidi ya Uswisi ilikuwa ni Julian Alvarez aliyefunga bao la kiwango cha juu na kuivunja ngome ya wapinzani.
Mshambuliaji huyo wa Atletico Madrid ameonekana kurejesha nafasi yake ya kwanza kikosini, huku Lautaro Martinez akiendelea kuwa tishio kutoka benchi baada ya kufunga bao la tatu mwishoni mwa mchezo.
Alvarez hupenda kukimbia kwenye nafasi za pembeni, jambo linalomfanya kipa Emiliano Martinez mara nyingi kupiga mipira mirefu kuelekea kwake.
Hivyo, England italazimika kushinda mipira ya kwanza na ya pili ili kumzuia Alvarez pamoja na Messi kupata nafasi za kushambulia.
Kiungo Leandro Paredes sasa amepewa jukumu la kukaa mbele ya mabeki, akiwapa uhuru zaidi Mac Allister na Enzo Fernandez kupanda mbele.
Dhidi ya Uswisi, Mac Allister, Enzo na Rodrigo De Paul hawakuwa kwenye kiwango chao bora.
Mabeki wa kati Cristian Romero na Lisandro Martinez wana uwezo wa kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma, ni wagumu kwenye kukaba na pia ni hatari wanapopanda kwenye mipira ya adhabu.
3. Nguvu, kasi na presha ndiyo silaha ya kuifunga Argentina
Uswisi iliwapa shida Argentina kwa kutumia nguvu, kasi na presha kubwa, hadi pale walipobaki wachezaji 10 baada ya Breel Embolo kutolewa kwa kadi nyekundu.
Baada ya mchezo huo, Scaloni mwenyewe alikiri kuwa timu yake ilipoteza mapambano mengi ya mmoja dhidi ya mmoja.
Isipokuwa Paredes, viungo wengi wa Argentina hawapendi kucheza mchezo wa mabavu.
Kama Granit Xhaka na Remo Freuler waliweza kuwabana, basi viungo wa England kama Declan Rice na Elliot Anderson wana uwezo wa kufanya hivyo pia, mradi timu nzima ishirikiane.
England pia inaweza kutumia kasi pembeni mwa uwanja, ambako Argentina imeonekana kuwa dhaifu.
Scaloni amekiri wazi kuwa mabeki wake wa pembeni si miongoni mwa bora duniani.
Ndiyo maana Dan Ndoye wa Uswisi aliwasumbua mara kadhaa kabla ya kufunga bao la kusawazisha kwa ushirikiano mzuri na wenzake.
4. Argentina hupoteza umakini kirahisi
Tabia nyingine ambayo England inaweza kuitumia ni namna Argentina inavyolegeza mchezo baada ya kupata bao la kuongoza.
Mara nyingi hushindwa kujifunza kutokana na makosa yao ya kupoteza mipira ovyo na kuwaruhusu wapinzani kurejea mchezoni.
Ni kama timu hiyo hupenda drama ili icheze vizuri zaidi.
5. Mashabiki ni silaha nyingine ya Argentina
Kila mechi ambayo Argentina inacheza huhisi kama ipo nyumbani.
Mashabiki wao husafiri kwa idadi kubwa na huungwa mkono na watazamaji wengi wanaokuja kumuona Messi na kushuhudia mazingira ya kipekee yanayozunguka timu hiyo.
Sapoti hiyo huwapa wachezaji nguvu ya ziada, hasa wanapokuwa kwenye kipindi kigumu cha mchezo.
Kwa Waargentina, soka si mchezo tu, bali ni sehemu ya utambulisho wao.
6. England itulie, lakini icheze kwa moyo
Mchezo dhidi ya Argentina una historia kubwa na unatarajiwa kuwa wa presha kubwa ndani na nje ya uwanja mjini Atlanta.
England italazimika kulingana na wapinzani wao kwa nguvu, kasi na kujituma, lakini bila kupoteza nidhamu.
Iwapo itabaki pungufu kwa kadi nyekundu, inaweza kujikuta ikirudia maumivu ya mwaka 1998 badala ya kuandika historia mpya mwaka 2026.
Kwa upande mwingine, England inaweza pia kutumia presha hiyo kuwavuruga wachezaji wenye hasira za haraka kama Cristian Romero, na kuwafanya wajigharimishe wenyewe kwa kufanya makosa yatakayobadili kabisa mwelekeo wa mchezo.