Tuchel 'achekelea' kuiua Juventus

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa Chelsea, Thomas Tuchel amesisitiza kuwa wachezaji wake wanatakiwa kuendelea kuwa fiti na kuonyesha ubora mkubwa baada ya kutimiza mchezo wake wa 50 akiinoa timu hiyo kwa staili ya namna yake kufuatia kuishushia kipigo Juventus cha mabao 4-0.

Usiku wa jana, Jumanne ulikuwa mchungu kwa mashabiki wa Juventus kwani chama lao lilikumbana na kipigo kikubwa kwenye historia ya ushiriki wao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Tuchel alisema hayo kutokana na mtiani mzito walionao mbele yao kuhakikisha wanatetea taji lao la Ligi ya Mabingwa  Ulaya.

"Ilikuwa mechi nzuri sana kuwa mechi ya 50. Ni juhudi gani, ni mtazamo gani. Kufunga mabao mengi dhidi ya timu inayolinda vizuri ni mafanikio ya ajabu. Ni muhimu sasa kufurahia."

"Jumatano ni siku ya mapumziko na wanastahili kabisa kisha kuanzia Alhamisi tutajiandaa kwa mechi inayofuata. Tutaweka miguu  sawa  lakini ilikuwa mechi kali bila shaka."

Mabao matatu ya kwanza ya Chelsea yalifungwa na wahitimu wa akademi ya timu hiyo, Trevoh Chalobah, Reece James na Callum Hudson-Odoi kabla ya Timo Werner kuongeza la nne dakika za mwishoni mwa mchezo huo ambao ulichezwa kwenye uwanja wa Stamford Bridge.

Tuchel alisema; "Hiki ndicho kinachoifanya timu kuwa maalum. Sio tu magwiji na wachezaji bora kutoka nje ambao pia tunao kwenye kikosi chetu bali ni mchanganyiko.

"Kuwa na vijana wenye vipaji, wanyenyekevu kutoka katika akademi iliyojaa ubora na ni ndoto yao kubwa kucheza Stamford Bridge, kuwa sehemu ya timu imara ya Chelsea hii ni nzuri sana kuwa sehemu yake.

Majeraha ya goti yaliyowapata Ben Chilwell na N'Golo Kante ni ishara mbaya kwa Chelsea ambayo wikiendi ijayo itakuwa na kibarua cha kucheza dhidi  ya dhidi ya Manchester United.

Kuhusu Chilwell, ambaye alichechemea kipindi cha pili, Tuchel alisema; 'Inanitia wasiwasi kwa sababu alikuwa katika wakati mzuri kama Reece upande ule mwingine.

"Walikuwa katika umbo bora zaidi wangeweza kuwa, wenye nguvu sana, waliojaa kujiamini na ubora mwingi.

"Alikuwa na maumivu makali, sasa anajisikia vizuri zaidi. Tutamfanyia vipimo kesho (leo, Jumatano)  ili kuwa sahihi zaidi. Tunatumai mema.'

Kuhusu Kante ambaye alitolewa katika kipindi cha kwanza, Tuchel aliongeza: 'Alikuwa sana tena mwenye nguvu katika kipindi cha kwanza na kisha akapata dhoruba kidogo ya  goti, nadhani atakuwa sawa, hayakuwa majeraha makubwa, ni kama mstuko alipata."

MATOKEO KWA UJUMLA


Dyn. Kyiv 1-2 Bayern Munich
Villarreal 0-2 Man Utd
Barcelona 0-0 Benfica
Chelsea 4-0 Juventus
Lille 1-0 Salzburg
Malmo FF 1-1 Zenit
Sevilla 2-0 Wolfsburg
Young Boys 3-3 Atalanta