Tuchel aamua Giroud abaki

Sunday June 06 2021
tuchel pic

LONDON, ENGLAND. NDO hivyo. Uamuzi wa Kocha Thomas Tuchel kumwongezea mkataba mpya straika Olivier Giroud unatajwa huenda ni meseji tosha kutoka kwa Chelsea bado hawapo tayari kwenye vita ya kumnasa Harry Kane.

Straika wa Tottenham, Kane aliweka wazi anataka kuachana na timu hiyo kwa ajili ya kwenda kujiunga na timu itakayompa nafasi ya kubeba mataji kitu ambacho Chelsea iliingia kwenye mchakato wa kunasa saini yake.

Lakini, kumpa mkataba mpya Giroud kunatoa maana Tuchel bado hajaamua juu ya kunasa fowadi mpya.

Kocha huyo Mjerumani amebadili mfumo tangu alipotua Stamford Bridge, Januari mwaka huu na kwenye safu ya ushambuliaji alikuwa akimpa nafasi kubwa zaidi Timo Werner, lakini baada ya kuona mabao hayapatikani, Giroud alipewa nafasi wakati mwingine alitumia mtindo wa kutumia Namba 9 bandia.

Kwenye mtindo wa Namba 9 bandia, kuna wachezaji kadhaa walitumika kwenye staili hiyo, akiwamo Kai Havertz na Christian Pulisic. Hivyo, kwa dili jipya la Giroud - hiyo ina maana Tuchel atakuwa na wigo mpana wa uteuzi kwenye safu yake ya ushambuliaji kwa msimu ujao.

Hapo Tammy Abraham hajahusishwa, akibaki machaguo yatakuwa mengi zaidi licha ya kwamba straika huyo kinda amekuwa akihusishwa na mpango wa kuachana na maisha ya Stamford Bridge kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Advertisement

Kuhusu Giroud alikuwa akihusishwa na timu za AC Milan, lakini sasa ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho.

Advertisement