Trump asema hajali Iran ikijitoa Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Marekani na Israel zilianza kushambulia majengo ndani ya Iran Jumamosi Februari 28, 2026, huku mzozo wa Mashariki ya Kati ukizidi kuenea katika eneo zima.
NEW YORK, MAREKANI: RAIS wa Marekani, Donald Trump amesema hajali kama Iran itashiriki Kombe la Dunia 2026 au la, ambalo litaandaliwa kwa pamoja na Marekani, Mexico na Canada wakati wa majira yajayo ya kiangazi.
Marekani na Israel zilianza kushambulia majengo ndani ya Iran Jumamosi Februari 28, 2026, huku mzozo wa Mashariki ya Kati ukizidi kuenea katika eneo zima.
Rais Trump ameliambia Gazeti la Politico: “Kwa kweli sijali. Nadhani Iran ni nchi iliyoshindwa vibaya sana. Wanaendelea kwa shida.”
Iran ndiyo ilikuwa taifa pekee lililokosekana katika mkutano wa mipango wa FIFA kwa ajili ya washiriki wa Kombe la Dunia uliofanyika wiki hii jijini Atlanta, jambo lililoongeza maswali kama timu yao itashiriki nchini Marekani wakati huu wa vita vinavyozidi kupamba moto katika eneo hilo. FIFA haikutoa maoni mara moja ilipoombwa kutoa ufafanuzi.
Mehdi Taj, Rais wa Shirikisho la Soka la Iran, amesema ukali wa mashambulizi ya Marekani na Israel hauashirii vyema maandalizi ya Kombe la Dunia, litakalofanyika kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, 2026.
Iran ilijihakikishia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia 2026 kwa mara ya nne mfululizo baada ya kuongoza Kundi A katika raundi ya tatu ya kufuzu ya kupitia Asia mwaka jana. Iran imepangwa Kundi G pamoja na Ubelgiji, Misri na New Zealand. Mechi zao zimepangwa kufanyika Marekani, mbili jijini Los Angeles na moja jijini Seattle.
Iwapo Marekani na Iran zitamaliza katika nafasi ya pili kwenye makundi yao, zinaweza kukutana katika hatua ya 32 bora, Julai 3 katika Uwanja wa AT&T, ulioko Arlington, Texas.
Iran ni moja ya mataifa mawili yanayoshiriki Kombe la Dunia 2026 yaliyoathiriwa na marufuku kali zaidi ya usafiri iliyowekwa na Trump kupitia amri ya kiutendaji, Juni mwaka jana, kwa mujibu wa Politico.
Ingawa marufuku hiyo inaziruhusu timu za Kombe la Dunia na wafanyakazi wao wa kusaidia, maamuzi kuhusu visa kwa wengine wakiwemo maafisa wa serikali au watendaji wa makampuni yanayodhamini timu yatafanywa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa kila kesi kivyake.
Andrew Giuliani, mkurugenzi wa Kikosi Kazi cha Ikulu cha Kombe la Dunia cha FIFA, amesema katika mahojiano ya Januari kwamba masuala ya usalama yataongoza maamuzi ya serikali kuhusu ruhusa za kipekee za kusafiri.
Katika enzi ya kisasa, hakuna timu iliyofuzu Kombe la Dunia iliyokosa kushiriki fainali zake. Iwapo Iran itajiondoa, karibu bila shaka itabadilishwa na taifa jingine.