TRIONDA: Mpira wa ‘AI’ Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Mpira huo unaoitwa Adidas Trionda unauzwa takriban Dola 160 ukiwa umetengenezwa kwa namna ambayo haisaidii tu wachezaji, bali pia waamuzi kwani ndani yake kuna teknolojia inayosaidia katika uamuzi ya ‘offside’.
NYON, SWITZERLAND: SHIRIKISHO la Kandanda Duniani (Fifa) limezindua mpira utakaotumika katika Kombe la Dunia 2026 ambao una maboresho kibao ya kiteknolojia ikiwemo akili unde (AI).
Mpira huo unaoitwa Adidas Trionda unauzwa takriban Dola 160 ukiwa umetengenezwa kwa namna ambayo haisaidii tu wachezaji, bali pia waamuzi kwani ndani yake kuna teknolojia inayosaidia katika uamuzi ya ‘offside’.
Rangi zake ni nyeupe, nyekundu, bluu na kijani zikibeba alama za mataifa yatakayokuwa wenyeji wa mashindano ambayo ni Marekani, Canada na Mexico na kwa mwonekano unafanana kidogo na ule mpira wa Brazuca uliotumika katika Kombe la Dunia 2014 kule Brazil.
Mpira huo una nyota ya bluu ambayo inawakilisha Marekani, jani jekundu la ua la maple linalo wakilisha Canada na pia kuna tai wa kijani kama alama ya Mexico
Sam Handy, makamu wa rais wa Adidas anayeshulika na ubunifu amesema: “Huu ndio mpira wa Kombe la Dunia ulio na mwonekano wa kuvutia zaidi tuliowahi kutengeneza. Tumeuandaa kwa kuzingatia kwamba utatumika katika mashindano makubwa zaidi duniani na ubora wake hautakufanya uishie kuutazama tu, bali utatamani kuucheza, kuushika na kuutazama.”
Ndani ya mpira huo kuna ‘chip’ maalumu ambayo inatuma taarifa moja kwa moja kwenye mfumo wa VAR.
Vilevile mpira huo umefungwa kifaa maalumu ambacho kinakusanya taarifa ikiwa ulishikwa mkononi na ikiwa mchezaji aliyekuwa nao aliotoea au la.
Katika matangazo ya uzinduzi, nyota wa Real Madrid, Jude Bellingham Lionel Messi wa Inter Miami na Lamine Yamal wa Barcelona walionekana wakifurahia kuuchezea.
Mojawapo wa picha ilimuonyesha Lamine Yamal akiwa ameshika mpira mkubwa mno na baadaye baadhi ya mashabiki wakaanza kusema atawezaje kuutumia kucheza, lakini Fifa ikatoa ufafanuzi kwamba huo ulikuwa ni mfano.
Hata hivyo, mipira ya mashindano ya hivi karibuni ukiondoa ule wa Kombe la Dunia 2014, mara nyingi imekuwa ikikosolewa na wachezaji kuwa na uelekeo tofauti pale inapopigwa kwenda juu.
“Mpira huu umeundwa kwa ajili ya tukio kubwa zaidi la michezo duniani. Huu ni mpira wa kwanza wa aina yake ukiwa na teknolojia ya maalumu na umeunganishwa na mfumo wa AI ili kutoa data na taarifa za papo kwa papo zitakazosaidia kila kitu kuanzia uamuzi wa waamuzi hadi uchambuzi wa matukio,” imesema taarifa ya Adidas.