Trent Alexander-Arnold aingia anga za Man City
Muktasari:
- Beki huyo amekuwa akihusishwa kutaka kuondoka katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid tangu kuanza kwa dirisha hili la usajili huko Ulaya.
MANCHESTER City inaendelea kumfuatilia kwa karibu beki wa kulia wa Real Madrid na timu ya taifa ya England, Trent Alexander-Arnold, 27.
Beki huyo amekuwa akihusishwa kutaka kuondoka katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid tangu kuanza kwa dirisha hili la usajili huko Ulaya.
Taarifa zinaeleza kuwa Man City inavutiwa na uwezo wa Trent katika kupandisha mashambulizi na inaami inaweza kuipata huduma yake ikiwa itawasilisha ofa nono kwa waajiri wake wa sasa.
Hatma ya nyota huyo katika viunga vya Bernabeu bado haijawekwa wazi, jambo linalozifanya timu kadhaa kubwa Ulaya kuendelea kumnyemela.
Inaelezwa kwamba Real Madrid itakuwa tayari kumwachia mchezaji huyo ikiwa itawasilishiwa ofa nono.
Inaaminika kwamba mabosi wa timu hiyo wanaamini kuwa nyota huyo haendani na timu yao, kwani licha ya kurudishwa nyuma kutokana na majeraha ya mara kwa mara, lakini hata pale anapopata nafasi ya kucheza kiwango chake hakionekani kuvutia.
Man City inataka huduma ya mchezaji huyo katika dirisha hili la usajili kutokana na idadi kubwa ya majeruhi kwenye mabeki tegemeo katika kikosi cha kwanzacha miaka hiyo.
Real Madrid bado haijatoa msimamo wa moja kwa moja kuhusu mustakabali wa beki huyo, lakini iko tayari kuzisikiliza timu mbalimbali zinazomtaka mchezaji huyo wa zamani wa Liverpool.
Rayan
BOURNEMOUTH iko karibu kukamilisha usajili wa mshambuliaji chipukizi wa Vasco da Gama na timu ya taifa Brazil, Rayan Vitor Simplício Rocha, 19, kwa mkataba wa kudumu.
Mchezaji huyo amekuwa na kiwango bora tangu msimu uliopita ambapo alicheza mechi 57 za michuano yote na kufunga mabao 20.
Dili hilo linatajwa kufikia hatua za mwisho, huku pande zote zikiwa na matumaini ya kukamilisha kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Mkataba wake unamalizika 2028.
Tim Iroegbunam
LAZIO imewasilisha ofa inayoweza kufikia Pauni 15 milioni kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Everton na England, Tim Iroegbunam, 22.
Timu hiyo ya Serie A inaamini Iroegbunam anaendana na mfumo kutokana na uchezaji wake wa matumizi ya nguvu.
Everton bado haijathibitisha ikiwa imekubali ofa hiyo au la, na mazungumzo bado yanaendelea ikielezwa mabosi wa timu hiyo wanataka dau liongezwe. Mkataba wa Iroegbunam unatarajiwa kumalizika 2027.
Mohamed Kader Meite
CHELSEA na Manchester United zinamfuatilia kwa karibu mshambuliaji chipukizi wa Rennes na Ufaransa, Mohamed Kader Meite, 18.
Timu hizo mbili za Ligi Kuu England zilituma maskauti kwenda kumtazama Meite akicheza mara kadhaa katika Ligi Kuu Ufaransa, na taarifa zinaonyesha zimevutiwa naye.
Rennes inamwona kuwa mchezaji muhimu katika mipango yake, hivyo inahitaji ofa inayoikia Pauni 40 milioni.
Jeremy Jacquet
RENNES imekataa ya Chelsea iliyowasilisha katika dirisha hili la Januari kwa ajili ya kumsajili beki wa kati na timu ya taifa ya Ufaransa chini ya miaka 21, Jeremy Jacquet, 20.
Hata hivyo, Chelsea bado haijakata tamaa inaendelea kumfuatilia na ikishindwa sasa itarudi katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Tangu kuanza kwa msimu huu Jacquet amecheza mechi 18 za michuano yote. Mkataba wake wa unatarajiwa kumalizika 2029.
Othmane Maamma
LIVERPOOL, Manchester United na Newcastle United zinaendelea kumfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa Watford na timu ya taifa ya Morocco, 20, Othmane Maamma.
Staa huyo amevutia macho ya maskauti wengi wa vigogo hao ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu.
Watford inatajwa kuwa tayari kumuuza, lakini kwa klabu ambayo itayowasilisha ofa nono dirisha hili au lijalo la majira ya kiangazi.
Giorgio Scalvini
NEWCASTLE United inaendelea kufanya mazungumzo na Atalanta kwa ajili ya kumsajili staa wa timu hiyo na timu ya taifa ya Italia, Giorgio Scalvini, 22, kwa ajili ya kumsajili katika dirisha hili ili akawe mbadala wa beki raia wa Uswisi, Fabian Schar, 34, ambaye amepata majeraha yanayotarajiwa kumuweka nje kwa muda mrefu. Scalvini anasifika kwa uwezo mkubwa wa kusoma mchezo.
Jonas Omlin
KIPA wa Borussia Monchengladbach na timu ya taifa ya Uswisi, Jonas Omlin, 32, amekataa ofa ya kujiunga na Sunderland katika dirisha hili na badala yake anataka kujiunga na Bayer Leverkusen iliyo tayari kumsajili kwa mkopo hadi mwisho wa msimu.
Omlin alikuwa akihusishwa kwenda Sunderland, lakini ofa ya Leverkusen inaonekana kumvutia zaidi kutokana na kumpa nafasi ya katika michuano ya kimataifa.