Tony Woodcock kupata medali ya Ulaya baada ya miaka 46 ya kusubiri
Muktasari:
- Tony Woodcock kupata medali ya Ulaya baada ya miaka 46 ya kusubiri
SALFORD, ENGLAND: MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa England, Tony Woodcock, hatimaye anatarajiwa kupokea medali yake ya ushindi wa Kombe la Ulaya baada ya miaka 46 tangu aliponyimwa mwaka 1980 akiwa sehemu ya kikosi cha Nottingham Forest kilichoshinda taji hilo mwaka uliotangulia.
Woodcork alianza katika fainali dhidi ya Malmo, kisha akacheza mechi nne msimu uliofuata wa mashindano hayo.
Hata hivyo, aliondoka klabuni kabla ya Forest kutetea ubingwa kwa ushindi dhidi ya Hamburger SV katika fainali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Namna alivyotoka klabuni ilisababisha mvutano kati yake na Kocha Brian Clough, jambo lililosababisha anyimwe medali baada ya timu kunyanyua kombe. Woodcock amesema wakala wake alijaribu mara kadhaa kuwasiliana ili apate medali hiyo, lakini hakupata majibu.
Sasa, baada ya miaka mingi, atakabidhiwa medali hiyo katika hafla itakayofanyika kabla ya mchezo wa robo fainali ya Europa League kati ya Forest na Porto, keshokutwa, Alhamisi.
Akizungumza na The Times, Woodcock, 70, alisema: "Nilikuwa nimeachana na jambo hilo zamani kwa sababu tulidhani hakuna kitakachotokea. Lakini, kadri unavyozeeka na kupata hekima unaanza kufikiria, Mungu wangu, nilikuwa na mchango mkubwa katika hilo na ninastahili kutokana na mechi nilizocheza.
"Hivyo nikasema nitarudi kulifuatilia. Sipendi watu waseme kwamba mimi si mshindi wa Kombe la Ulaya."
Awali, kulikuwa na mpango wa Chama cha Soka England kumpa medali hiyo kabla ya mechi ya England katika Uwanja wa Wembley, lakini ikaamuliwa apewe mbele ya mashabiki wa Forest. Katika maisha yake ya soka, Woodcock alifunga mabao 16 katika mechi 42 alizochezea England.
Woodcock alipitia akademi ya Forest kabla ya kupanda hadi kikosi cha kwanza na kukisaidia kushinda ubingwa wa ligi 1978.
Hata hivyo, Brian Clough alimshutumu kwa kudai mshahara mkubwa alipokuwa akitakiwa kusaini mkataba mpya na uhusiano wao mbaya ulichangiahata klabu kuzuia uhamisho wake kwenda FC Koln. Baadaye aliruhusiwa kuondoka na aliwahi pia kuchezea Arsenal na Fortuna Koln.