Aston Villa yaishtaki FIFA kwa CAS
Muktasari:
- Klabu ya Aston Villa imewasilisha rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kupinga uamuzi wa FIFA wa kuzuia usajili wa mshambuliaji chipukizi Brian Madjo, mwenye umri wa miaka 17.
LONDON, ENGLAND: ASTON Villa yaifikisha FIFA Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) baada ya kuzuiwa kumsajili chipukizi Brian Madjo.
Klabu ya Aston Villa imewasilisha rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kupinga uamuzi wa FIFA wa kuzuia usajili wa mshambuliaji chipukizi Brian Madjo, mwenye umri wa miaka 17.
Villa inadaiwa kulipa euro12 milioni 12, mwezi Januari ili kumsajili Madjo kutoka klabu ya Metz ya Ufaransa. Hata hivyo, tangu awasili England, ameshindwa kuichezea Villa kutokana na FIFA kukataa kumpa kibali cha kucheza.
Kwa nini FIFA imekataa usajili?
Kanuni za FIFA zinazuia uhamisho wa kimataifa wa wachezaji walio chini ya umri wa miaka 18, jambo lililomzuia Madjo kusajiliwa rasmi. Mchezaji huyo atatimiza miaka 18 mwezi Januari mwakani.
Chanzo kikuu cha mgogoro huo ni kwamba sheria za FIFA zinaruhusu wachezaji wenye umri wa miaka 16 au 17 kuhamia klabu nyingine ndani ya Umoja wa Ulaya (EU). Hata hivyo, baada ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya (Brexit), klabu za England hazinufaiki tena na msamaha huo.
Kesi tayari imeanza kusikilizwa
Mahakama ya CAS imethibitisha kuwa usikilizwaji wa rufaa ya Aston Villa ulifanyika Jumatano, lakini bado haijatangaza tarehe ya kutoa uamuzi.
Villa inatarajia kupata hukumu mapema kutokana na msimu mpya kukaribia. Klabu hiyo itashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, huku mwisho wa kuwasilisha orodha ya wachezaji kwa UEFA ukiwa Septemba 2, siku moja baada ya kufungwa kwa dirisha la usajili la England.
Madjo hajacheza tangu Desemba
Brian Madjo alicheza mechi yake ya mwisho ya mashindano akiwa na Metz katika Ligue 1 mwezi Desemba mwaka jana.
Kimataifa, aliwahi kuichezea Luxembourg katika mechi za kirafiki za timu ya wakubwa kabla ya kubadili uraia wa kisoka na sasa anaiwakilisha England katika timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
Sasa Aston Villa inasubiri uamuzi wa CAS, ambao utaamua ikiwa chipukizi huyo ataruhusiwa kuanza kuitumikia klabu hiyo au ataendelea kusubiri hadi atakapofikisha umri wa miaka 18.