Toney, Galeno waibua kashfa Saudi Arabia, waitaja Al Nassr
Muktasari:
- Kwa sasa, Al-Nassr ya Ronaldo inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili huku zikiwa zimesalia mechi saba na endapo watafanikiwa kutwaa ubingwa itakuwa taji la kwanza la ligi kwa Ronaldo tangu ajiunge na klabu hiyo.
RIYADH, SAUDI ARABIA: MWAMBA kachokonolewa. Mshambuliaji wa kimataifa wa England, Ivan Toney anayekipiga Ah Ahli ya Saudi Arabia ametoa mashambulizi makali dhidi ya uadilifu wa uamuzi wa waamuzi katika Saudi Pro League, huku mmoja wa wachezaji wenzake akidai kuna jitihada za “kukabidhi ubingwa” kwa Cristiano Ronaldo.
Toney alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Al-Ahli waliolalamikia uamuzi wa waamuzi baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Al-Fayha wiki hii, matokeo yaliyowaacha nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, pointi mbili nyuma ya Al-Nassr ya Ronaldo, ambayo inaongoza ikiwa pia na mechi moja mkononi.
Toney aliyefunga bao lake la 27 msimu huu katika mechi hiyo, alidai timu yake ilinyimwa penalti kadhaa na walipojaribu kuzungumza na mwamuzi waliambiwa waelekeze fikra zao kwenye Ligi ya Mabingwa Asia (AFC) badala ya mechi hiyo.
“Kulikuwa na matukio mawili ya wazi ya penalti, na ni wizi wa mchana kweupe,” amesema Toney baada ya mechi.
“Tulipojaribu kuzungumza na mwamuzi alituambia tuzingatie AFC. Inawezekanaje aseme hivyo wakati tunazungumzia mechi hii?”
Amesema uamuzi huo unazua maswali hasa katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea mwisho wa msimu na kusisitiza, “Hizi zilikuwa penalti za wazi, lakini sasa tumefika hatua muhimu wanabadilisha mambo.”
Alipoulizwa nani anaweza kunufaika na uamuzi huo, Toney alicheka na kusema: “Tunajua tunamfukuza nani?” kauli ambayo wengi wameitafsiri kuwa inamrejea Ronaldo.
Baadaye, Toney aliongeza msimamo wake kupitia mitandao ya kijamii akichapisha video za matukio matatu anayodai zilikuwa penalti za wazi na kuandika, “ni wazi kuna kitu kinaathiri uamuzi huu.”
Mchezaji mwenzake, Wenderson Galeno naye alizua mjadala akidai ligi hiyo inataka ‘kumpa ubingwa mtu mmoja.’
“Wanataka kututoa kwenye mbio za ubingwa kwa njia yoyote na kumpa kombe mtu mmoja, hii ni dharau kubwa kwa klabu yetu,” aliandika. Al-Ahli ilisimama nyuma ya wachezaji wake ikitoa taarifa ikilalamikia makosa ya waamuzi na kudai uwazi zaidi, ikiitaka ligi kutoa rekodi za mawasiliano kati ya waamuzi na VAR pamoja na maelezo ya wazi kuhusu uamuzi uliochukuliwa.
Kwa sasa, Al-Nassr ya Ronaldo inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili huku zikiwa zimesalia mechi saba na endapo watafanikiwa kutwaa ubingwa itakuwa taji la kwanza la ligi kwa Ronaldo tangu ajiunge na klabu hiyo.