Tonali ageuka habari ya mjini Ulaya
Muktasari:
- Maskauti wa mabingwa hao wa La Liga walihudhuria mechi ya FA Cup ambayo Newcastle ilifungwa mabao 3-1 na Man City katika Jumamosi.
NEWCASTLE, ENGLAND: VIGOGO wa soka Ulaya wamezidi kuongezeka kuhitaji kumsajili kiungo wa Newcastle United, Sandro Tonali baada ya Real Madrid kuungana na Arsenal, Manchester City, Manchester United na Arsenal.
Maskauti wa mabingwa hao wa La Liga walihudhuria mechi ya FA Cup ambayo Newcastle ilifungwa mabao 3-1 na Man City katika Jumamosi.
Inaelezwa wawakilishi wa Madrid walikuwepo kiwanjani hapo wakichunguza mbinu za kuishinda Man City ya Pep Guardiola kabla ya miamba hiyo miwili kukutana hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza wajumbe wa Madrid walikuwa na lengo la pili la kumtazama kiungo huyo wa Italia mwenye umri wa miaka 25.
Ili kumpata fundi huyo, Madrid itatakiwa kuingia kwenye vita ya usajili dhidi ya Man City, Man United na Arsenal ambazo pia zimeonyesha nia ya kumsajili licha ya Newcastle kuhitaji takriban Pauni 100 milioni ili kumuuza.
Mwaka uliopita Newcastle ilimuuza mshambuliaji wake Alexander Isak kwa Pauni 130 milioni ambayo ilivunja rekodi ya ada ya usajili ya England.
Taarifa Tonali tayari ameonyesha nia ya kubaki msimu ujao hazijathibitishwa ingawa inaelezwa pia hadi sasa bado hajawasilisha ombi lolote la kutaka kuondoka.
Moja ya mambo yanayoweza kumzuia kuondoka ni mke wake Juliette aliyejifungua mtoto wa kiume aitwaye Leonardo Januari mwaka huu na familia yake inaishi kwa furaha Kaskazini Mashariki mwa England, hivyo kwa sasa itakuwa changamoto kuisumbua kuhama.
Kwa sasa Newcastle inataka kupambana kumbakisha Tonali katika viunga vya St James' Park na hawana presha kwani kiungo huyo ana mkataba unaomwezesha kukunja Pauni 150,000 kwa wiki unaodumu hadi mwaka 2030.
Hata hivyo, klabu inafahamu Tonali mwenyewe anaweza akawasilisha maombi ya kutaka kuondoka ikiwa watashindwa kufuzu kucheza mashindano ya Ulaya, pia kujitokeza kwa Madrid kutaka kumsajili inaweza kuwa jambo gumu kwake kukataa.