Thoms Partey ana dili mezani
Muktasari:
- Staa huyo wa kimataifa wa Ghana amezifikisha mwisho zama zake kwenye kikosi cha Arsenal alikocheza kwa miaka mitano baada ya mkataba wake kufika tamati mwishoni mwa msimu wa 2024-25.
LONDON, ENGLAND: ALIYEKUWA kiungo wa Arsenal, Thomas Partey yupo kwenye hatua za mwisho kabisa za kukamilisha dili lake la kujiunga na Villarreal, imeelezwa.
Staa huyo wa kimataifa wa Ghana amezifikisha mwisho zama zake kwenye kikosi cha Arsenal alikocheza kwa miaka mitano baada ya mkataba wake kufika tamati mwishoni mwa msimu wa 2024-25.
Siku nne baada ya kuondoka Arsenal, Partey alifunguliwa mashtaka matano ya tuhuma za kuwabaka wanawake wawili tofauti na kumfanyia unyanyasaji mwanamke mwingine wa tatu.
Partey, ambaye alikanusha kufanya makosa hayo, alikamatwa kwa mara ya kwanza Julai 2022, lakini kesi hiyo ilikuwa haijatajwa na mchezaji huyo alikuwa akiendelea kuitumikia Arsenal wakati uchunguzi ukiwa unaendelea.
Na sasa, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32, anapaswa kufika kwenye mahakama ya hakimu mkazi ya Westminster, Jumanne, Agosti 5.
Na sasa, kiungo huyo wa zamani wa Ligi Kuu England anaripotiwa kwenye kwenye hatua za mwisho za kujiunga na Villarreal ya Hispania.
Alishafanya vipimo vya afya na anatarajia kusaini mkataba wa miaka miwili hadi 2027. Partey ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Arsenal kufika tamati Juni 30 na hakupewa dili jipya.
Kiungo huyo wa zamani wa Atletico Madrid alikuwa kwenye mazungumzo ya kuendelea kubaki Emirates, lakini makubaliano yalishindwa kufikiwa. Partey alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha kocha Mikel Arteta, ambapo kwa msimu wa 2024-25, alicheza mechi 52 za michuano yote. Kwa ujumla, Partey alifunga mabao tisa na kuasisti mara saba katika mechi 167 alizocheza tangu alipojiunga mwaka 2020.
MAVITU YA PARTEY HUKO ARSENAL EPL 2024-2025
-Amecheza: Mechi 35
-Ametengeneza: Nafasi 20
-Amefunga: Mabao 4
-Ametoa: Asisti 2
-Amelala takolin: Mara 89
-Amepiga: Pasi 1840