Madrid yatwaa ubingwa wa 36 La Liga

Muktasari:

  • Madrid imetwaa ubingwa huo zikisalia mechi nne kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa La Liga, huku ikiiacha Girona inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 13.

Real Madrid imeshinda ubingwa wa La Liga msimu huu 2023/24 ikiwa ni mara ya 36 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Cadiz.

Madrid imetwaa ubingwa huo zikisalia mechi nne kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa La Liga, huku ikiiacha Girona inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 13.

Licha ya kwamba Madrid ilipata ushindi mapema leo, lakini ilikuwa inasubiri matokeo ya Barcelona kujihakikishia ubingwa huo ambapo wapinzani wao hao wamekuja kufungwa mabao 4-2 na Girona, ndipo Madrid ikatangazwa mabingwa kwa tofauti ya pointi 14 dhidi ya Barcelona.

Girona iliyopo nafasi ya pili na Barcelona ya tatu, hata zikishinda mechi zao nne za mwisho, huku Madrid ikipoteza zote, hawataweza kukaa juu.

Brahimi Diaz (dk 51), Jude Bellingham (dk 68) na Joselu (dk 90+3), ndiyo waliofunga mabao hayo ya Madrid na kubeba ubingwa baada ya kufikisha pointi 87 baada ya kucheza mechi 34.

Taji hilo la La Liga ni la pili kwa Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti kushinda na timu hiyo, huku likiwa ni la sita katika ligi tano tofauti alizofundisha ambazo ni La Liga (2), Premier (1), Bundesliga (1), Ligue (1) na Serie A (1).

Ubingwa huo wa leo umekuja na rekodi kadhaa ikiwemo ya kiungo mkongwe wa timu hiyo, Luka Modrić kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kucheza mechi ya La Liga akiwa na kikosi cha Real Madrid. Modric amecheza akiwa na miaka 38 na siku 238, akiipiku rekodi ya Ferenc Puskás (miaka 38 na siku 233).

Bao la Jude Bellingham katika mchezo huo limemfanya kufikisha jumla ya mabao 22 na asisti 10 katika michuano yote ukiwa ni msimu wake wa kwanza kikosini hapo.

Ilishuhudiwa pia urejeo wa kipa namba moja wa kikosi hicho, Thibaut Courtois ambaye amecheza kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kukosekana tangu Agosti 2023 alipoumia ambapo awali ilielezwa angeweza kuukosa msimu mzima.

Wakati Courtois akiwa nje akiuguza majeraha kabla ya kupona, Andriy Lunin ameifanya kazi kwa usahihi akiifikisha timu hiyo nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akisaidiana na Kepa Arrizabalaga.

Tayari Ancelotti amebainisha kuwa mwenye namba yake golini kwa maana ya Courtois amerejea na atacheza mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano ijayo dhidi ya Bayern Munich baada ya ile ya kwanza ugenini kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.