Tatu zajitokeza dili la Jack Grealish

Muktasari:
- Inaelezwa Manchester City inahitaji kiasi cha Pauni 40 milioni kama ada ya uhamisho ya staa huyu.
TOTTENHAM, Newcastle na Napoli zipo katika vita ya kuiwania saini ya kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya England, Jack Grealish dirisha hili.
Inaelezwa Manchester City inahitaji kiasi cha Pauni 40 milioni kama ada ya uhamisho ya staa huyu.
Grealish ni miongoni mwa wachezaji walioonyeshewa mlango wa kutokea dirisha hili kwa sababu hayupo katika mipango ya Kocha Pep Guardiola.
Man City inataka kumwondoa pia ili kupunguza bili ya mshahara kwani licha ya kutokuwa katika mipango ya Pep, pia ni mmoja wa mastaa wanaolipwa pesa nyingi Ligi Kuu England.
Timu nyingi zimeripotiwa kuwasilisha maombi ya kutaka kumsajili kwa mkopo kutokana na kiwango cha ada ya uhamisho kinachohitajika lakini vigogo wa Man City wamekataa kwani wanataka kumuuza mazima.
Victor Osimhen
NAPOLI imekataa ofa ya Euro 60 milioni kutoka Galatasaray inayohitaji huduma ya mshambuliaji wao wa kimataifa wa Nigeria mwenye umri wa miaka 26 Victor Osimhen. Vigogo wa Napoli wamekataa kiasi hicho cha pesa kwa sababu wanahitaji Euro 75 milioni ambazo ndizo zimewekwa katika mkataba wa Osimhen kwa timu yoyote itakayohitaji kumsajili.
Marc Guehi
NEWCASTLE United bado ina matumaini ya kushinda vita ya kumsajili beki wa kati wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Marc Guehi, 24, katika dirisha hili. Mabosi wa Newcastle wanaamini staa huyu atasaidia sana kuboresha safu yao ya ulinzi lakini imekuwa ngumu kumpata kutokana na wingi wa timu kubwa zinazomhitaji ambazo zimeweka ofa nono mezani.
Ousmane Diomande
CRYSTAL Palace ipo katika mazungumzo na Sporting Lisbon kwa ajili ya kumsaji beki wa kati wa timu hiyo na Ivory Coast, Ousmane Diomande, mwenye umri wa miaka 21, katika dirisha hili. Sporting ipo tayari kumuuza Diomande ambaye pia anahusishwa na vigogo mbalimbali barani Ulaya lakini inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 45 milioni kama ada ya uhamisho.
Nayef Aguerd
BEKI wa West Ham na timu ya taifa ya Morocco wa West Ham, Nayef Aguerd, mwenye umri wa miaka 29, yupo kwenye rada za Marseille ya Ufaransa inayohitaji kumsajili katika dirisha hili. Marseille inapambana kuboresha kikosi chao kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao kuanzia ligi ya ndani na michuano ya kimataifa.
Ederson
MANCHESTER United imewasiliana na Atalanta kuhusu kumsajili kiungo wao na timu ya taifa ya Brazil, Ederson, ambaye huduma yake pia inahitajika na Inter Milan na Juventus. Staa huyu mwenye umri wa miaka 26 anauzwa kwa kiasi kisichopungua Pauni 44 milioni.
Man United inaonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kukamilisha dili hili.
Rasmus Hojlund
Mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya Denmark, Rasmus Hojlund, 22, hana mpango wa kuondoka kwenye timu dirisha hili, isipokuwa kama ikiamua kumuuza. Kwa sasa Inter Milan inatajwa kuwa moja kati ya timu zinazohitaji huduma yake na ipo tayari kutoa zaidi ya Pauni 40 milioni kama ada yake ya uhamisho.
Andre Onana
MANCHESTER United inahitaji Pauni 30 milioni dirisha hili kwa ajili ya kumuuza kipa wake, Andre Onana dirisha hili. Taarifa mbalimbali zinadai AS Monco inatamani sana huduma ya fundi huyu lakini kiasi hicho cha pesa kinachotajika na Man United kama ada ya uhamisho ni kikubwa sana kwao. Kipa huyu wa kimataifa wa Cameroon anahusishwa kuondoka kutokana na kiwango chake.