Tajiri wa Napoli ataka mechi zipigwe dk 50
Muktasari:
- De Laurentiis amefurahia mafanikio ya hivi karibuni katika soka la Italia, huku klabu yake ikiwa mabingwa wa Serie A kwa mara nyingine tena baada ya kumaliza ukame wa miaka 33 bila taji. Napoli ilishinda tena ubingwa wa Ligi Kuu Italia 2022-23 na pia uliopita.
NAPLES, ITALIA: MMILIKI wa Klabu ya Napoli, Aurelio De Laurentiis, amependekeza mabadiliko makubwa katika soka akihofia kuwa mchezo huo utapoteza kizazi cha vijana ambacho kimekuwa kikipendelea mambo rahisi yasiyo na ugumu unaowafanya kuchoka haraka na kupuuza mambo au kutoyazingatia ipasavyo.
De Laurentiis amefurahia mafanikio ya hivi karibuni katika soka la Italia, huku klabu yake ikiwa mabingwa wa Serie A kwa mara nyingine tena baada ya kumaliza ukame wa miaka 33 bila taji. Napoli ilishinda tena ubingwa wa Ligi Kuu Italia 2022-23 na pia uliopita.
Hata hivyo, timu hiyo inaelekea kumaliza msimu huu bila taji kubwa ikiwa nafasi ya pili kwenye Serie A, lakini ikiwa nyuma kwa pointi tisa dhidi ya vinara Inter Milan huku zikiwa zimebaki mechi sita, na pia imetolewa kwenye Coppa Italia na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akihofia mustakabali wa mchezo huo, mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 76 ametoa mapendekezo kadhaa ya kuvutia ili kuwavutia zaidi vijana waendelee kuvutiwa na soka, ambapo akizungumza na The Athletic, pendekezo lake la kwanza ni kupunguza muda wa mechi kutoka dakika 90 hadi 50.
Bosi huyo kubwa wa Napoli anasema inafaa viwepo vipindi viwili vya dakika 25 kila kimoja, huku akisisitiza muda halisi wa mchezo (in-play time) badala ya muda wa nyongeza mwishoni mwa kila kipindi akidai mbele ya safari vijana watachoshwa na hivyo kutofurahia soka kama ilivyo sasa.
“Namba moja, nitapunguza (muda wa mechi) kutoka dakika 45 kila kipindi hadi dakika 25. Pia huwezi kuendelea kujilaza uwanjani na kuigiza kama mwigizaji! Hapana, utatolewa nje,” anasema.
Pendekezo lake la pili ni kuondoa kabisa matumizi ya kadi za njano na nyekundu, na badala yake kutumia mfumo unaofanana na ule wa raga wa kuwatoa wachezaji nje kwa muda (sin-bin) na hii itamaanisha mchezaji akipata onyo ataondolewa kwa dakika tano kabla ya kurejea, huku kadi nyekundu ikimaanisha kuondolewa kwa dakika 20.
“Sitatumia kamwe kadi nyekundu au ya njano. Nitasema ‘wewe toka nje kwa dakika tano’ (kwa kosa la kawaida), na ‘wewe toka nje kwa dakika 20’ kwa kosa kubwa,” anasema akisisitiza kwamba mabadiliko yake ya mwisho yanahusu sheria ya kuotea (offside), jambo ambalo linaweza kuwafurahisha wakosoaji wengi.
Akitaka kuhamasisha mchezo wa kushambulia zaidi, anapendekeza washambuliaji wapewe nafasi kubwa zaidi ya kuhesabiwa hawajaotea wanapokuwa wanaelekea golini.
“Kitu kingine. Kuna mabao machache sana, hivyo mchezo hauvutii. Lazima kuwe na mabao mengi zaidi. Na ili kupata mabao mengi, lazima ubadilishe sheria. Huwezi kufuta bao kwa sababu ya milimita chache tu (za mtu kuotea)… sheria ya offside lazima ibadilishwe,” anasema De Laurentiis.
Alisisitiza umuhimu wa kuvutia kizazi kipya akisema: “Kizazi kipya ndicho dhahabu yetu. Tusipowaridhisha, tutapotea. (Mchezo huu) hautakuwa na ushiriki (mkubwa) kama uliokuwepo katika miaka 100 iliyopita.