Garnacho akiri makosa yake, asisitiza hana kinyongo
Muktasari:
- Tangu ajiunge na Chelsea, Garnacho amecheza mechi 37 katika mashindano yote na kufunga mabao manane akiwa na changamoto ya kupata nafasi ya kuanza mara kwa mara kwa sasa.
LONDON, ENGLAND: WINGA wa Chelsea, Alejandro Garnacho, amezungumza kwa mara pili kuhusu kuondoka kwake katika Manchester United akisema kuwa ingawa hatua hiyo ilimuumiza, lakini bado ana heshima na upendo mkubwa kwa klabu hiyo.
Mara ya kwanza mchezaji huyo alizungumza siku chache tu baada ya kuondoka Old Trafford, Juni 30, 2025, ambapo aliwalalamikia viongozi wa klabu hiyo kumlea aliyekuwa kocha wakati huo, Ruben Amorim kwamba ndiye aliyekuwa chanzo cha matatizo mengi na pia kuondoka kwake akiamini kwamba Mreno huyo hakuwa anamtendea haki.
Hata hivyo, akizungumza mara ya pili kuhusu kuondoka kwake amesema: “Pengine ndiyo kwa sababu niliipenda klabu hiyo. Walinipa imani tangu mwanzo, kulikuwa na upendo mkubwa kutoka kwa kila mtu, mashabiki, uwanja kila kitu kilikuwa kizuri sana.”
Garnacho aliondoka Old Trafford majira ya joto kwa ada ya Pauni 40 milioni baada ya mvutano na Amorim ambao ulianzia kukosa muda wa kutosha kucheza kwenye fainali ya Europa League dhidi ya Tottenham Hotspur iliyopigwa Mei 21, 2025, mechi ambayo Man United ililala kwa bao 1-0.
Kuhusu kipindi hicho kigumu alichopitia amesema: “Nilianza kukaa benchi, akilini mwangu nilihisi labda ni makosa yangu pia nikaanza kufanya baadhi ya mambo mabaya.”
Kabla ya kuondoka alizua mjadala baada ya kuchapisha picha akiwa amevaa jezi ya Aston Villa yenye jina la Marcus Rashford aliyekuwa anaichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Manchester United, jambo lililowakasirisha mashabiki wa Mashetani Wekundu na kuanza kumchukia wakitaka atimuliwe klabuni kwao.
Hata hivyo Garnacho alisisitiza kuwa hana kinyongo na Manchester United akisema: “Nina kumbukumbu nzuri tu za Manchester United. Sina majuto yoyote.”
Aliongeza kuwa wakati mwingine mchezaji hulazimika kubadilika kwa ajili ya hatua inayofuata ya maisha yake na ndicho hata yeye alitaka kitokee kwa sababu alipitia wakati mgumu ambao hata baadhi ya watu waliamini kwamba alikuwa hatendewi haki na kocha wake.
Katika kipindi cha Amorim nyota wengi wa timu hiyo walijikuta wakikwaruzana naye akiwamo Rashford ambaye licha ya kwamba alilelewa na Mashetani Wekundu katika makuzi ya soka, lakini kocha huyo alianza kumshambulia kwa mambo mengi binafsi na kufikia hatua kumtoa kwa mkopo Aston Villa kisha Barcelona anakowaka hivi sasa.
Uamuzi huo wa Amorim umemfanya Rashford aichukie Manchester United hadi sasa kiasi kwamba pamoja na kwamba kiwango chake kipo juu hataki kabisa kurejea Old Trafford hata baada ya mkopo wake, akitaka auzwe na klabu hiyo.
Wengine waliojikuta katika wakati mgumu wakati wa kocha huyo ni Jadon Sancho anayecheza kwa mkopo Aston Villa, Rasmus Hojlund aliyepo Napoli anakocheza kwa mkopo, Harry Maguire aliyekuwa akisugulishwa benchi na Kobbie Mainoo aliyerejea kikosi cha kwanza hivi sasa.
Tangu ajiunge na Chelsea, Garnacho amecheza mechi 37 katika mashindano yote na kufunga mabao manane akiwa na changamoto ya kupata nafasi ya kuanza mara kwa mara kwa sasa.
Hata hivyo, kocha wa kikosi hicho, Liam Rosenior amemsifu akisema: “Garna ni mchezaji wa kiwango cha juu… ni mchezaji bora sana… ana uwezo mkubwa na kipaji kikubwa. Anaonyesha maendeleo mazuri na anaweza kuwa mchezaji muhimu zaidi kwa Chelsea kadri anavyoendelea kupata nafasi."