Konate, Liverpool kuna jambo wanapika pembeni
Muktasari:
- Nyota huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa awali alitajwa kuwa huenda akaondoka katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu, lakini sasa kuna uwezekano mkubwa wa kubaki baada ya mazungumzo ya mkataba mpya kufikia hatua nzuri.
BEKI wa kati wa Liverpool, Ibrahima Konate, 26, yupo karibu kufikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Anfield.
Nyota huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa awali alitajwa kuwa huenda akaondoka katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu, lakini sasa kuna uwezekano mkubwa wa kubaki baada ya mazungumzo ya mkataba mpya kufikia hatua nzuri.
Inaelezwa kuwa Konate anaweza kusaini mkataba wa miaka minne kabla hata ya kwenda katika michuano ya Kombe la Dunia na Ufaransa.
Real Madrid na Bayern Munich ni miongoni mwa timu zilizokuwa zinahusishwa na nyota huyo na zilidaiwa kuanza mazungumzo na wawakilishi wake.
Katika mkataba huo mpya, Liverpool imempa Konate ofa ya mshahara mpya unaofikia Pauni 150,000 kwa wiki kutoka Pauni 70,000 kwa wiki anazopata hivi sasa.
Tangu kuanza kwa msimu huu, licha ya majeraha ya mara kwa mara, amecheza mechi 45 za michuano yote.
James Trafford
ASTON Villa imeingia katika vita dhidi ya klabu nyingi ili kuhakikisha inaipata saini ya kipa wa Manchester City na England, James Trafford, 23. Trafford aliyesajiliwa na Man City msimu uliopita, amekuwa na nafasi finyu katika kikosi cha kwanza ambapo benchi la ufundi linapendelea kumtumia Muitaliano Gianluigi Donnarumma, 27. Aston Villa inaamini Trafford anaweza kuvaa viatu vya kipa wao Emiliano Martinez ambaye hana mrefu kikosini hapo.
Anthony Gordon
BBAYERN Munich inataka kumsajili winga wa Newcastle United na timu ya taifa ya England, Anthony Gordon, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Gordon ambaye ameendelea kung’ara Ligi Kuu England zaidi ya misimu miwili amekuwa akitajwa kuwindwa na timu nyingi kubwa kuelekea dirisha lijalo. Bayern Munich inataka kuongeza nguvu katika maeneo ya pembeni na Gordon anaonekana kuwa chaguo linalofaa kwa kocha Vincent Kompany.
Nico Schlotterbeck
BEKI wa kati wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Nico Schlotterbeck, 26, anaripotiwa kuwa na kipengele maalumu cha kuvunja mkataba kinachoeleza timu inayomtaka itatakiwa kulipa kati ya Pauni 43 milioi hadi milioni 52. Kipengele hicho kinadaiwa kuzihusu klabu za nje ya Ujerumani jambo linalozipa nafasi Liverpool na Real Madrid. Mabosi wa Dortmundwanapambana kumsainisha mkataba mpya.
Bazoumana Toure
LIVERPOOL inaonyesha nia ya kumsajili winga wa TSG Hoffenheim na Ivory Coast, Bazoumana Toure, 20, katika dirisha la majira ya kiangazi baada ya kung’ara msimu huu. Liverpool inataka kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji, na inaamini Toure anaweza kuleta mabadiliko na kuongeza ushindani. Iwapo dili hilo litafanikiwa, nyota huyo anaweza kuwa sehemu ya kizazi kipya cha wachezaji wa Liverpool.
Cristian Romero
BEKI wa Tottenham Hotspur na Argentina, Cristian Romero, 27, anadaiwa kuwa ameshawaaga wachezaji wenzake kwamba ataondoka mwisho wa msimu. taarifa zinaeleza kuwa Spurs ipo tayari kumuuza kwa sababu inataka kuanza upya katika baadhi ya maeneo ya kikosi, jambo linaloweza kusababisha kuuzwa baadhi ya wachezaji muhimu. Romero amekuwa mmoja wa mabeki muhimu Spurs. Mkataba unamalizika 2029.
Jadon Sancho
WINGA wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Jadon Sancho, 26, atalazimika kukubali kupunguza mshahara ikiwa anataka kurejea Borussia Dortmund baada ya msimu huu kumalizika. Sancho aliwahi kung’ara akiwa Dortmund kabla ya kuhamia Manchester United, lakini tangu atue England amekuwa na panda shuka nyingi akicheza kwa mkopo Aston Villa.
Scott McTominay
NAPOLI inapanga kumuongezea mkataba kiungo raia wa Scotland, Scott McTominay, 29, kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu. McTominay ambaye hivi karibuni aliripotiwa huenda angerejea Ligi Kuu England mwisho wa msimu, tangu atue Napoli 2024 amekuwa mmoja kati ya wachezaji waliionyesha kiwango bora. Uongozi Napoli unataka kumlinda nyota huyo asiondoke.