Straika waiweka Arsenal njiapanda

Muktasari:
- Miamba hiyo ya Emirates imeweka kipaumbele kwenye usajili wa straika mpya katika dirisha lijalo baada ya kumaliza msimu bila ya taji lolote kwa msimu wa tano mfululizo.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL ipo njia panda kuhusu straika gani wa kumbeba kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya kati ya Benjamin Sesko na Viktor Gyokeres, imeelezwa.
Miamba hiyo ya Emirates imeweka kipaumbele kwenye usajili wa straika mpya katika dirisha lijalo baada ya kumaliza msimu bila ya taji lolote kwa msimu wa tano mfululizo.
Arsenal imeweka mezani jina la straika wa RB Leipzig, Sesko na wa Sporting Lisbon, Gyokeres kwenye orodha ya mastraika inaowasaka baada ya kuona ishu ya kumnasa Alexander Isak kutoka Newcastle United kuwa ngumu. Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi David Ornstein, klabu hiyo ipo njiapanda.
Alibainisha, Arsenal imefanya kazi kubwa kwenye ishu ya kumsajili Sesko, lakini kuna mambo machache yamebaki kukamilika pengine kwenye ada na makubaliano binafsi ya mchezaji.
Taarifa za kutoka Ujerumani zinafichua Sesko, 21, bei yake anayouzwa ni Pauni 62 milioni kulingana na kipengele kilichochomekwa kwenye mkataba wake na kuna timu nyingine zinamtaka pia ikiwamo Chelsea, Manchester United na Tottenham.
Na kuhusu Gyokeres, 26, kwenye mkataba wake kumechomekwa kipengele kinachohitajika kulipwa Pauni 85 milioni, lakini klabu yake ya Sporting ipo tayari kupokea ada ya Pauni 60 milioni.
Arsenal inapaswa kufanya haraka kunasa saini ya straika huyo kama inamtaka kabla ya ushindani kuwa mkali kutokana na klabu nyingine kuingia vitani kunasa huduma yake.
Ornstein alisema: “Gyokeres ni chaguo bora kutokana na pesa anayouzwa, lakini muda unakimbia na timu nyingine zinaweza kuingia na kama Arsenal inamtaka afanye haraka sasa kuliko kuendelea kusubiri.”
Kocha wa Man United, Ruben Amorim anatamani kuungana tena na straika wake huyo wa zamani baada ya kufanya kazi kwa mafanikio Sporting, lakini Atletico Madrid inamtaka pia. Gyokeres yupo kwenye kurasa za mbele za magazeti ya Ureno ikidaiwa kwamba amepewa ofa ya mshahara wa Pauni 7 milioni kwa mwaka na klabu ya Arsenal. Lakini, miamba hiyo inayonolewa na Mikel Arteta bado haijapeleka ofa rasmi ya kumsajili mshambuliaji huyo.
Mkuu wa maskauti wa Arsenal walipaswa kwenda kutazama mechi ya Sporting na Benfica iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 Jumamosi iliyopita lengo lilikuwa kwenye kumtazama Gyokeres. Lakini, wachezaji wengine waliotazamwa kwenye mechi hiyo ni Ousmane Diomande na Francisco Trincao.
Beki wa kati Diomande, 21, kwa muda mrefu amekuwa kwenye rada za klabu za Ligi Kuu England. Na winga Trincao, 25, ameanza kusakwa ghafla baada ya kufunga mabao 10 na kuasisti mara 18 msimu huu.