Staa wa Arsenal afutiwa kadi nyekundu
Muktasari:
- Kinda huyo wa Arsenal alitolewa kwa kadi nyekundu katika dakika 43 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, Jumamosi baada ya kumchezea rafu beki wa Wolves, Matt Doherty. Lewis-Skelly alimzuia beki huyo wa Wolves kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza baada ya Arsenal kupiga kona ya ovyo iliyookolewa kirahisi na Wolves kuanza kuandaa shambulizi la kaunta.
LONDON, ENGLAND: KADI nyekundu aliyoonyeshwa mchezaji wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly imeripotiwa ilitolewa kimakosa na sasa adhabu yake imefutwa, FA imetangaza.
Kinda huyo wa Arsenal alitolewa kwa kadi nyekundu katika dakika 43 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, Jumamosi baada ya kumchezea rafu beki wa Wolves, Matt Doherty. Lewis-Skelly alimzuia beki huyo wa Wolves kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza baada ya Arsenal kupiga kona ya ovyo iliyookolewa kirahisi na Wolves kuanza kuandaa shambulizi la kaunta.
Alionyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Michael Oliver - jambo ambalo lilimfanya kocha Mikel Arteta na wachezaji wa Arsenal kukasirika.
Arsenal ilikata rufaa FA na sasa adhabu ya Lewis-Skelly imefutwa.
Taarifa ya FA ilisomeka: "Kamati huru ya sheria imeeleza kwamba kuna kosa limefanyika kwenye kumtoa mchezaji Myles Lewis-Skelly na hivyo kuondoa adhabu yake ya kufungiwa mechi tatu. Mchezaji huyo wa Arsenal alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kucheza rafu mbaya kwenye mechi yao ya Ligi Kuu England dhidi ya Wolverhampton Wanderers, Jumamosi, Januari 25, 2025."
Mabosi wa kampuni inayosimamia waamuzi wa kulipwa (PGMOL) imefuata utaratibu kama iliyoufanya kwa kiungo wa Manchester United, Bruno Fernandes - ambaye alionyeshwa kadi nyekundu kimakosa kwenye mechi dhidi ya Tottenham Hotspur, Septemba mwaka jana.
Mwamuzi Oliver alikumbana na meseji za vitisho baada ya kadi nyekundu hiyo na kuwafanya polisi kuingia kwenye uchunguzi huku wakiimarisha ulinzi nyumbani kwa refa huyo. Oliver alitarajia kuchezesha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Barcelona na Atalanta usiku wa jana Jumatano.
Kwa maana hiyo, Lewis-Skelly, 18, sasa atatumika na Arsenal kwenye mechi yao ijayo dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu England, Manchester City, Jumapili.