Staa Chelsea afungiwa miaka minne, akata rufaa CAS
Muktasari:
- Nyota huyo tayari amekata rufaa dhidi ya uamuzi huo ambao sasa umefikishwa katika Mahakama ya Usuluhusi wa Masuala ya Michezo (CAS).
LONDON, ENGLAND: MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Mykhailo Mudryk amepewa adhabu ya kufungiwa miaka minne na Cham,a cha Soka England (FA), baada ya kupimwa na kukutwa na dawa iliyopigwa marufuku 2024, kwa mujibu wa taarifa za talkSPORT.
Nyota huyo tayari amekata rufaa dhidi ya uamuzi huo ambao sasa umefikishwa katika Mahakama ya Usuluhusi wa Masuala ya Michezo (CAS).
Desemba 2024, Mudryk alisimamishwa kwa muda na FA baada ya sampuli ya mkojo wake kuonyesha uwepo wa dawa iliyopigwa marufuku ya 'Meldonium' alipokuwa kwenye majukumu ya kimataifa ya nchi yake ya Ukraine.
Baada ya kusimamishwa kwa muda, FA ilimfungulia mashtaka mwezi Juni kufuatia uchambuzi wa sampuli ya pili (B Sample) kuonyesha uhalisia wa matumizi ya dawa hizo katika mkojo wake.
Adhabu hiyo ilimzuia mchezaji huyo kufanya mazoezi na Chelsea, na kutokana na hali hiyo amekuwa akitumia viwanja vya klabu ndogo ya Uxbridge FC katika kujiweka fiti kimwili.
Mudryk amekuwa akikanusha kufanya kosa lolote, na ameajiri kampuni ya kisheria ya Morgan Sports Law kusimamia suala hilo ambayo pia iliwahi kumsimamia staa wa zamani wa Manchester United na Juventus, Paul Pogba wakati wa adhabu yake ya matumizi ya dawa hizo.
Kesi ya rufaa ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 bado haijapangiwa kusikilizwa, ambapo anatarajia kufutiwa kabisa adhabu hiyo au angalau kupunguziwa iwapo atashinda au kuhurumiwa. Hali kama hiyo iliwahi kumtokea Pogba ambaye adhabu yake ya miaka minne ilipunguzwa hadi miezi 18, Oktoba 2024.
MUDRYK ANAWEZA KUREJEA LINI?
Adhabu ya mchezaji ambaye amecheza mechi 28 za kimataifa itahesabiwa kuanzia aliposimamishwa kwa muda, na inaweza kumuweka nje ya uwanja hadi mwaka 2028, ingawa tarehe kamili ya kurejea bado haijajulikana.
Mwandishi wa talkSPORT, Ben Jacobs, alisema pande zote bado zinawasilisha hoja kwa maandishi na kusubiri tarehe ya kusikilizwa kwa kesi.
Aliongeza kuwa Mudryk anatumia mawakili walewale wa Pogba akitarajia ama kuondolewa kabisa hatia na CAS au kupunguziwa adhabu. Ikiwa adhabu itapunguzwa kama ilivyokuwa kwa Pogba kuna uwezekano wa kurejea uwanjani kabla ya mwisho wa msimu ujao.
Lakini ikiwa CAS itapigilia msumari uamuzi wa FA na adhabu ya miaka minne kubaki, basi mustakabali wake ndani ya Chelsea na hata katika soka kwa ujumla unaweza kuwa shakani.
Jacobs pia alieleza kuwa Meldonium ni dawa inayoongeza nguvu na kusisimua mwili ikiwamo kusaidia kupona haraka na kuongeza stamina. Dawa hiyo pia iliwahi kutumiwa na mcheza tenisi Maria Sharapova.
Hata hivyo, Mudryk anasisitiza kuwa hakutumia dawa yoyote kwa makusudi. Changamoto kubwa ni kwamba wanamichezo wanawajibika moja kwa moja kwa chochote kinachoingia mwilini mwao hata kama ni kwa bahati mbaya.
HASARA YA MKWANJA
Adhabu ya Mudryk pia ni pigo kwa klabu yake ya zamani, Shakhtar Donetsk, ambayo inaweza kupoteza Euro 30 milioni ikiwa hataichezea tena Chelsea.
Mudryk alijiunga na Chelsea Januari 2023 kwa ada ya awali ya Euro 70 milioni pamoja na nyongeza ya Euro 30 milioni kulingana na mafanikio ya klabu na mchango wake - fedha ambazo bado hazijalipwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shakhtar, Sergei Palkin, alisema klabu hiyo itapoteza fedha hizo ikiwa mchezaji huyo hatarejea uwanjani. Mudryk alicheza mara ya mwisho kwa Chelsea, Novemba 2024, katika mechi ya Europa Conference League dhidi ya Heidenheim ya Ujerumani.