Ghana 'wamenyongwa' Kombe la Dunia
Muktasari:
- Kocha huyo wa Ghana alisisitiza kuwa timu yake ilipaswa kupewa penalti mwishoni mwa mchezo huo wakati Prince Kwabena Adu alipokuwa akikimbilia ndani ya eneo la hatari kabla ya Ezri Konsa kuingilia na kuonekana kumuangusha kiungo huyo.
DALLAS, Marekani: "Kwa mara nyingine tena VAR imeenda kunywa kahawa."
Wakati Ghana wakisherehekea suluhu waliyopata dhidi ya England, lakini kocha wao Carlos Queiroz hakuacha kujiuliza nini kingetokea kama uamuzi fulani ungetolewa tofauti.
Kocha huyo wa Ghana alisisitiza kuwa timu yake ilipaswa kupewa penalti mwishoni mwa mchezo huo wakati Prince Kwabena Adu alipokuwa akikimbilia ndani ya eneo la hatari kabla ya Ezri Konsa kuingilia na kuonekana kumuangusha kiungo huyo.
Hakuna penalti iliyotolewa, jambo lililowapa afueni mashabiki wa England. Marudio ya mchezo yalionyesha kuwa Konsa alimkanyaga Adu kwenye goti huku akiwa hajaugusa mpira.
Queiroz alisema “sina uhakika kama VAR bado inafanya kazi katika Kombe la Dunia. Bado tunayo VAR? Inafanya kazi kweli?
“Nina mashaka kuhusu hilo kwa sababu kulikuwa na penalti nyingine ambayo Ghana ilipaswa kupewa dhidi ya England,penalti ya wazi kabisa. Wao wana bahati. Wana bahati sana.
“Ilikuwa penalti ya wazi na kadi nyekundu pia. Je, mna mashaka yoyote kuhusu hilo? Ninyi mlioangalia mchezo mna mashaka yoyote, au ni mimi tu niliyekuwa uwanjani?
“Samahani kwa kejeli zangu, lakini nikisema mambo haya kwa uzito wanaweza kuniadhibu, hivyo natumaini mnaelewa kwamba natania.”
Wachambuzi wa BBC Sport waliokuwa wakifuatilia mchezo huo walikubaliana kwa kiasi kikubwa kwamba Konsa na England walikuwa na bahati kutoadhibiwa.
Mshambuliaji wa zamani wa England na Manchester United, Wayne Rooney, alisema kwenye BBC One:“Nadhani hiyo ilikuwa penalti.
“Konsa alichukua hatari kubwa. Miguu yake ilikuwa hewani alipokuwa akijirusha na alimgonga mchezaji, si mpira.
“Kwa maoni yangu, hiyo ingeweza kutolewa kwa urahisi kabisa.”
Mchezaji wa zamani wa England na Manchester City, Micah Richards, aliongeza: “England walikuwa wakisaka bao la ushindi, walikuwa wanajaribu kufunga, lakini bado unahitaji kuwa na ulinzi wa kutosha nyuma yako.
“Siku nyingine, hiyo ingeweza kuwa penalti.”
Iwapo tukio hilo lilikuwa penalti ya wazi kama wengi wa waliotazama wanavyoamini, kwa nini halikuchunguzwa na mwamuzi msaidizi wa video (VAR)?
Katika Ligi Kuu England, huenda tukio kama hilo lingechunguzwa upya, lakini katika Kombe hili la Dunia matumizi ya VAR yanafanyika kwa namna tofauti kidogo.
Pierluigi Collina, ambaye ni mkuu wa waamuzi wa FIFA, anataka kuwe na kiwango cha juu zaidi kabla ya kuingilia uamuzi ya mwamuzi wa uwanjani, pamoja na kuhakikisha kunakuwa na uthabiti katika utoaji wa uamuzi.
Mantiki yake ni kwamba ikiwa waamuzi wanaruhusu michezo mingi kuendelea bila kupuliza faulo uwanjani, basi pia kunapaswa kuwa na idadi ndogo ya uingiliaji wa VAR.
Huenda hiyo ndiyo sababu iliyofanya kuonekana kwamba hakukuwa na mapitio ya VAR kuhusu tukio hilo maalum.
Darren Cann, ambaye alikuwa mwamuzi msaidizi katika fainali ya Kombe la Dunia 2010, anaamini kuwa uamuzi usio sahihi ulifanyika.
Akizungumza kwenye BBC Sport alisema: “Kama shabiki wa England ninafurahi kwamba penalti hiyo haikutolewa.
“Lakini lazima niwe mkweli, kwa maoni yangu tukio hili lilipaswa kurejelewa kwa VAR...
“Konsa hakuugusa mpira kabisa. Alimwangusha mpinzani wake.
“Alikuwa ameruka hewani, hakuwa tena na udhibiti wa mwili wake, na akamgusa mshambuliaji.
“Kwa maoni yangu, hii ilikuwa penalti ya wazi.”