Staa avunjika mifupa ya shingo, hatarini kupooza
Muktasari:
- Nyota huyo mwenye umri wa miaka, 31, aliyekuwa akiichezea klabu yake Guangxi Pingguo katika mechi dhidi ya Chongqing Tonglianglong katika ligi daraja lapili nchini China alipata ajali mbaya baada ya kujigonga katika bango na kuvunjika shingo.
BEIJING, CHINA: NYOTA wa kimataifa wa Togo, Samuel Asamoah yupo katika hatari kubwa ya kupooza mwili mzima baada ya kujigongana vibaya katika bango la matangazo Uwanjani.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka, 31, aliyekuwa akiichezea klabu yake Guangxi Pingguo katika mechi dhidi ya Chongqing Tonglianglong katika ligi daraja lapili nchini China alipata ajali mbaya baada ya kujigonga katika bango na kuvunjika shingo.
Video iliyorekodiwa wakati wa mechi hiyo, iliyochezwa Jumapili iliyopita, ilionyesha Asamoah akigombania mpira na kiungo wa timu pinzani, Zhang Zhixiong na katika harakati hizo, Asamoah alionekana akijigonga kwa kichwa kwenye bango lililoko kando ya uwanja kisha akadondoka chini kabla ya madaktari kwenda kumtibu.
Baada ya tukio hilo, siku moja baadae, klabu yake ilitoa taarifa ya kushtua ikisema staa huyo yupo katika hatari kubwa ya kupooza mwili mzima baada ya mifupa mingi shingoni mwake kuvunjika na kukata mishipa ya neva.
Klabu hiyo ilithibitisha kuwa Asamoah alifanyiwa upasuaji na atakosa mechi zote zilizobaki msimu huu, na kuongeza kuwa , anaweza asionekane tena kiwanjani.
"Guangxi Pingguo FC inashukuru kwa dhati mashabiki wote na watu wengine kwa kuwa na wasiwasi na kuonyesha nia ya kutaka kutoa msaada kwa Samuel Asamoah. Maendeleo ya hali yake yatatangazwa siku zijazo baada ya vipimo zaidi."
Asamoah, ambaye ameichezea Togo katika mechi sita za kimataifa, alitumia sehemu kubwa ya maisha yake ya soka kucheza Ubelgiji kabla ya kuhamia Romania mwaka 2021, kisha kutua China mwaka 2024 kujiunga na Qingdao Red Lions kwa msimu mmoja kabla ya kujiunga na klabu yake ya sasa.
Tukio hili linafananishwa na lile la nyota wa zamani wa akademi ya Arsenal, Billy Vigar ambaye alifariki mwezi uliopita baada ya kukaa kwenye koma kwa siku 10 kutokana na jeraha kubwa la ubongo.
Vigar, 21, anadaiwa kuwa alipata jeraha hilo baada ya kichwa chake kugonha ukuta wa zege kando ya uwanja wakati akiicheza Chichester City inayoshiriki ligi ya madaraja ya chini England.