Hebu sikia hii ya Asamoah Gyan
Muktasari:
- Gyan, 39, alianzia kucheza soka Liberty Professionals mwaka 2003 kabla ya kunaswa na Udinese kwa ada ambayo haikuwekwa wazi. Gyan alitumikia miaka mitano huko Italia, ambapo pia alitolewa kwa mkopo Modena kati ya 2004 na 2006, kabla ya kutimkia Rennes.
LONDON, ENGLAND
SIKIA hii. Staa Asamoah Gyan amevuna pesa nyingi sana kwenda Chinese Super League lakini lisemwalo kwa sasa, Mghana huyo ana Pauni 597 tu kwenye akaunti yake ya benki.
Gyan, 39, alianzia kucheza soka Liberty Professionals mwaka 2003 kabla ya kunaswa na Udinese kwa ada ambayo haikuwekwa wazi. Gyan alitumikia miaka mitano huko Italia, ambapo pia alitolewa kwa mkopo Modena kati ya 2004 na 2006, kabla ya kutimkia Rennes.
Baada ya kufunga mabao 14 katika mechi 51 katika kikosi cha Rennes, Sunderland ilivunja rekodi yake ya uhamisho ilimponasa Gyan kwa Pauni 10 milioni mwaka 2010, lakini kwenye timu hiyo hakudumu sana, alitolewa kwa mkopo kwenda Al Ain mwaka 2011 kabla ya kutua jumla kwenye timu hiyo mwaka uliofuatia.
Gyan alikuwa akivuna Pauni 160,000 kwa wiki huko United Arab Emirates, mara tatu ya kile alichokuwa akilipwa Sunderland na mshahara aliufanyia kazi alifunga mabao 112 katika mechi 107.
Mwaka 2015, Gyan aliboresha kipato chake baada ya kuhamia Shanghai SIPG chini ya kocha Sven-Goran Eriksson.
Huko China, Gyan aliripotiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanane wanaolipwa mshahara mkubwa duniani, ambapo alikuwa akilipwa Pauni 227,000 kwa wiki.
Hata hivyo, Gyan alifunga mabao manane katika mechi 26 kwenye kikosi hicho na mashabiki kuona kama pesa aliyokuwa akilipwa haiendani na kiwango chake. Straika huyo alizichezea pia Kayserispor, NorthEast United, na Legon Cities kabla ya kustaafu mwaka 2021 - huku akifunga mabao 51 katika mechi 109 alizochezea timu ya taifa ya Ghana. Na wakati Gyan akidaiwa kuvuna pesa nyingi kwenye soka, supastaa huyo alidaiwa mwaka 2018 kuwa na Pauni 597 tu iliyobaki kwenye akaunti yake ya benki, aliambia MyNewsGh.com: "Mbele, nyuma, juu chini, hiyo ndiyo pesa niliyonayo."