Spurs dua kama zote Arsenal iichape Bayern

LONDON, ENGLAND.UMESIKIA hii? Eti mashabiki wa Tottenham Hotspur kisiri siri wanataka Arsenal iichape Bayern Munich wiki ijayo ili kuweka hai matumaini yao ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao wakiwa namba tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

England inapewa nafasi kubwa ya kuwa moja ya nchi zitakazokuwa na mwakilishi wa ziada kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Na hilo litawezekana kama timu zake zilizopo kwenye michuano ya Ulaya msimu huu zitashinda na kusonga hatua zinazofuata ili kuwaongezea pointi kwenye msimamo wa viwango Uefa.

Lakini, kwenye mechi za kwanza za hatua ya robo fainali, Liverpool ilikumbana na kichapo cha mabao 3-0 nyumbani mbele ya Atalanta, wakati Bayer Leverkusen iliichapa West Ham 2-0 kwenye mechi nyingine ya Europa League na kuweka wasiwasi mkubwa wa kupeleka timu tano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kwenye mechi ya kwanza Arsenal ilitoka 2-2 na Bayern, wakati wawakilishi wengine wa Ligi Kuu England, Manchester City wenyewe walitoka sare ya mabao 3-3 na Real Madrid huko Bernabeu.

Na sasa kinachosubiriwa ni matokeo za marudiano kuona kitatokea nini, huku Ujerumani ikiwa na nafasi ya kuishusha England kwenye viwango vya Uefa na hivyo kunufaika wenyewe kwenye nafasi za ziada kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kwa timu za England, Aston Villa pekee ndiyo iliyoshinda mechi yake ya kwanza ilipoichapa 2-1 Lille kwenye Conference League na hilo linaiweka njia hiyo kuwa na nafasi ya kuwa na timu mbili kwenye Europa League. Kila ushindi, sare na kusonga raundi inayofuatia kwa kila timu inaongeza pointi kwa nchi yao na kutoa nafasi ya kuwa na timu ya ziada kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na michuano mingine ya Uefa msimu ujao.

Lakini, ushindi wowote kwa timu za Ujerumani zitakuwa na faida kubwa kuzidi kwa Ligi Kuu England. Kama Arsenal itashinda Allianz Arena, sambamba na ushindi wa Man City kwa Real Madrid huko Etihad na Aston Villa ikikwepa kipigo huko Ufaransa, England itakuwa kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa Uefa.

Lakini, ushindi kwa Bayern na Leverkusen ikikwepa kipigo hali itakuwa mbaya, labda kama Liverpool itafanya kweli dhidi ya Atalanta na hapo itahitajika Man City iichape Real Madrid na kisha iende kuitoa Bayern Munich kwenye nusu fainali, hapo itakuwa imesaidia England kuwa na pointi za kutosha kwenye chati za Uefa.

Kabla ya mechi za jana, Spurs ilikuwa kwenye nafasi ya nne katika msimamo, lakini ushindani ni mkali na yenyewe inapambana isitoke nje ya Top Five.